RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi lakini bado kazi ya kukabiliana na janga hilo ni kubwa.
“Ni mapambano magumu lakini kuna dalili kama tunashinda kwa sababu hali ya leo ni tofauti kabisa na hali ilivyokuwa miaka 10 iliyopita,” Rais Kikwete alisema, Juni 19, 2013 Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Rais Kikwete alikuwa akizungumza na baadhi ya viongozi wakuu wa zamani wa Afrika ambao wanaunda taasisi iitwayo Mabingwa wa Kupambana na Ukimwi (AIDS Champions) Marais Wastaafu Festus Mogae wa Botswana na Benjamin William Mkapa pamoja na Profesa Miriam Were kutoka Kenya.
Rais Kikwete aliwaambia viongozi hao katika mkutano huo uliofuatiwa na chakula cha usiku, “Tumepata mafanikio mengi sana lakini mapambano yenyewe bado kabisa – kwa sababu bado kuna changamoto mbili kubwa – moja ni kuzuia maambukizi mapya na pili kuhakikisha wote ambao wameathirika wanaendelea kupatiwa dawa za kurefusha maisha.”
Rais Kikwete alisema kuwa kampeni ya kupima afya zao ili kujua kama watu wameathirika ama la inakwenda vizuri na kuwa mpaka sasa Watanzania milioni 18 wamepima afya zao tokea Julai 2007 wakati Rais Kikwete na Mama Salma Kikwete walipopima afya zao hadharani katika mkutano wa hadhara Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
“Imekuwa ni kampeni yenye mafanikio makubwa. Siku ile ya kwanza tulipima jumla ya watu 11,000 na tokea siku ile mpaka leo kiasi cha Watanzania milioni 18 wamepima, kiasi cha watu 653,000 wanatumia dawa na kwa hakika aibu iliyokuwa inahusishwa na ugonjwa wenyewe imepungua sana na inaendelea kupungua,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kazi yetu kubwa pia iliyoanza na ambayo tutaifanya kwa miaka mitano ijayo ni kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa akinamana waja wazito na pia kupunguza kabisa maambukizi mapya kwa watu wazima. Kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni shughuli ambayo tunaifanya chini ya programu yetu ya miaka mitano.”
Rais Mogae alimpongeza Rais Kikwete na Serikali yake kwa mafanikio hayo makubwa katika kupambana na ugonjwa ambao unakadiriwa kuwa umeteketeza maisha ya Watanzania milioni mbili tokea ulipoingia nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980.
“Kwa hakika sote katika Afrika tumetoka mbali sana. Tumepoteza watu wengi sana. Tumepoteza vijana wengi mno. Nakupongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yako kwa kufikia hatua hii,” Rais Mogae alimwambia Rais Kikwete.
Naye Rais Mkapa alimwomba Rais Kikwete kushauriana na viongozi wenzake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) juu ya nchi hizo kushirikiana katika kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa za kurefusha maisha kwa waathirika kwa ukimwi.
“Mheshimiwa Rais lingekuwa jambo zuri kama nyinyi viongozi wa Afrika Mashariki mngeangalia uwezekano wa kujenga kiwanda cha dawa za ukimwi. Hili lingepunguza mzigo wa fedha wa kupatikana kwa dawa hizo kutoka nje na pia wakati mwingine hatuwezi kuwa na uhakika kuwa tutaendelea kupata fedha za kutosha za kuagiza dawa hizo huko mbele.”