Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kwenye Mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam uliowakutanisha wadau hao wa uchaguzi na kuwakumbusha wajibu wao katika jamii hususani katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi mkuu.
Alisema kuwa taasisi za kidini zinaaswa kama walivyo wadau wengine katika kipindi hiki cha uchaguzi kuhubiri amani na kuendelea kutoa elimu kwa watanzania ili zoezi hili liishe kwa amani na kuwaacha watanzania wakiwa na umoja na mshikamano licha ya tofauti za kiimani zilizopo miongoni mwao.
“Tume inawataka, nyinyi viongozi wa dini, mnapotoa mafundisho ya uchaguzi kwa waumini wenu kuhakikisha hamuonyeshi hisia za kuwa upande wa chama chochote cha kisiasa na zaidi kuepuka kushawishi waumini wenu kuegema chama au mgombea fulani,” amesema Jaji Lubuva.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Askofu Philemon Phiri wa kanisa la EAGT – Mikocheni -A ameiasa Tume hiyo kusimama katika haki, uhuru na kuhakikisha wanatangaza washindi bila kuonyesha upendeleo ili kuivusha nchi ikiwa salama.
Mshiriki mwingine kutoka Kanisa la Moravian Mchungaji Alamu Kajuna alisema kuwa amani ndiyo tunu kwa kila mwanadamu, hatutegemei vurugu wakati huu wa uchaguzi maana amani inapotoweka wanaoumia ni wananchi wakiwamo waumini wao hivyo wao kama taasisi zinazoshirikiana na wananchi kwa karibu kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi ili tupate viongozi kwa amani
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekutano na viongozi hao na wadau wengine ikiwa zimebaki siku mbili kuanza kwa kampeni hapo Jumamosi ijayo kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao.