Tume ya Mabadiliko ya Katiba Yapendekeza Uraia wa Nchi Moja

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,Jaji Joseph Warioba.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,Jaji Joseph Warioba.

Licha ya Rasimu ya Katiba kupendekeza muundo wa Serikali tatu, imetamka kuwa uraia utaendelea kuwa ni wa nchi moja ambayo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwasilisha Rasimu ya Katiba Bungeni jana, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema kuwa tume imependekeza suala la uraia kubaki kuwa la nchi moja kwa sababu moja ya masuala makuu ya kidola ni uraia.

Alisema uraia ni msingi wa utambulisho unaompa raia haki ya kulindwa na nchi yake, ikiwa ni pamoja na haki zake za binadamu za asili na zisizoondosheka kama zilivyotambuliwa au zitakavyotambuliwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba za nchi washirika na mikataba ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, Rasimu ya Katiba imependekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na wa kujiandikisha ambao katika kujiridhisha kwake ni uraia wa nchi moja usiojenga au kuleta hisia za kuwabagua au kuwatega raia katika matabaka na madaraja yanayotokana na tofauti ya hali au fursa zao.

Aidha, alisema rasimu hiyo imependekeza kuwapatia hadhi mahsusi watu wenye asili au nasaba ya utanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania kwa kuchukua uraia wa nchi nyingine lengo ni kuwarahisishia watu wenye asili ya Tanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine wakija nyumbani wasipate usumbufu na pia ili warahisishiwe ushiriki wao katika ujenzi wa taifa kwa kuwawezesha kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.

 

SOURCE: NIPASHE