Tume ya Kidato cha IV Yatoa Mapendekezo 130

Mwenyekiti wa Tume, Profesa Sifuni Mchome

TUME ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012, imetoa mapendekezo 130, mojawapo ikitaka kupitiwa upya kwa mitalaa ya elimu nchini.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alisema likitaka mitalaa ya shule za msingi hadi vyuo vya ualimu itazamwe upya. Tume hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari 23, mwaka huu kuchunguza chanzo cha asilimia 65.5 ya wanafunzi kupata daraja la sifuri kwenye mtihani wa mwaka 2012.

Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu baada ya Tume kumaliza kazi yake Juni 15 mwaka huu.

“Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado inaendelea,” alisema Profesa Mchome.

Alisema kwa kawaida mtalaa unabadilishwa baada ya kumaliza mzunguko wake mmoja, hivyo tume hiyo imependekeza kupitiwa upya kwa mitalaa yote ambayo imemaliza mzunguko. Mzunguko huu ni miaka saba kwa elimu ya msingi, minne kwa sekondari na miwili kwa kidato cha tano na sita.

“Mtalaa wa sekondari unaweza kupitiwa upya baada ya miaka minne tangu kuanza kutumika kwake, huu wa Sekondari wa ‘based competence’ (kuangalia ubora) ulianza kutumika 2006, mpaka sasa tayari umemaliza mzunguko wake na haya matokeo yametokana na mtalaa huu.

Tume imependekeza mitalaa yote itazamwe upya kuanzia ile ya shule za msingi mpaka vyuo vya ualimu,” alisema. Kuhusu vitabu, Tume imependekeza kuangaliwa kwa njia rahisi ya kutumia teknolojia kuhakikisha vinapatikana badala ya kusubiri mpaka vichapishwe na kisha kupelekwa kwa wanafunzi.

“Unaweza ukaongea na makampuni ya simu kuwa waweke vitabu kwenye system (mfumo) yao na wakaanza mashindano kuwa mwanafunzi atakayesoma sana atapata zawadi,” alisema na kuongeza.

“Unaweza pia kuongea na kampuni ya magazeti kama Mwananchi ukawaambia watoe ukurasa wachapishe kitabu fulani kwa mwezi mzima na shule ziambiwe zinunue nakala moja ambayo kwa mwezi itakuwa Sh30,000 kwa kila shule na tatizo la vitabu litakwisha.”

Pendekezo jingine alisema ni kuangaliwa upya kwa sheria mbalimbali za elimu jinsi zilivyo na utekelezwaji wake pamoja na kuhakikisha madaraka yanapelekwa kwenye ngazi za Serikali za Mitaa.
CHANZO: Mwananchi