Na Mwandishi Wetu
TUME ya Mabadiliko ya Katiba Oktoba 8, 2012 inatarajia kuanza awamu ya tatu ya kazi ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya katika Mikoa tisa (9) ikiwemo saba (7) ya Tanzania Bara na miwili ya Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid, Jijini Dar es Salaam, inaitaja Mikoa hiyo ni Mtwara, Kilimanjaro, Iringa, Singida, Njombe, Rukwa, Tabora, ambayo yote ni ya Tanzania Bara. Tume hiyo pia inatarajia kuitisha mikutano yake katika mikoa miwili ya Zanzibar, ambayo ni Kaskazini Unguja na Kaskazini Pemba.
Aidha taarifa hiyo inaongeza kuwa katika Mkoa wa Mtwara, Tumei taanza na Wilaya ya Nanyumbu, katika Mkoa wa Kilimanjaro Tume itaanza na Wilaya ya Moshi Mjini, katika Mkoa wa Iringa Tume itaanza katika Wilaya ya Mufindi. Kwa Mkoa wa Singida, Tume itaanza na Wilaya ya Iramba, wakati Mkoani Njombe, Tume itaanza na Wilaya ya Ludewa.
Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa katika Mkoa wa Rukwa Tume itaanzia katika Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Tabora Tume itaanza katika Wilaya ya Kaliua, Mkoa wa Kaskazini Unguja Tumeitaanza katika Wilaya ya Kaskazini “A” na Mkoa wa Kaskazini Pemba Tume itaanza katika Wilaya ya Wete.
Tume hiyo pia inawaomba wananchi kuhudhuria mikutano itakayoitishwa na Tume na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao binafsi kuhusu Katiba Mpya. Taarifa hiyo pia inawasisitiza wananchi wamikoa hiyo hasa wanawake na watu wenye ulemavu kutumia fursa ya kushiriki katika mikutano hiyo inayoitishwa na Tume ili kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya.