Tuienzi lugha ya Kiswahili kwa kuzungumza

20130725-195152.jpg

WAJUMBE wa Baraza la Katiba Manispaa ya Moshi, wamependekeza kuongezwa kwa wigo wa matumizi ya lugha ya Kiswahili na kutaka viongozi wa kitaifa kuhutubia kwa Kiswahili hata wawapo nje ya nchi.

“Sisi ndiyo tunaotakiwa kukienzi Kiswahili, lakini ni ajabu anakuja kiongozi wa China nchini anahutubia Kichina halafu Rais wetu yeye anahutubia kwa Kiingereza” alihoji Ali Mwamba.

Mwamba ambaye ni mjumbe kutoka Kata ya Korongoni, alikuwa akitoa maoni yake jana mjini Moshi mbele ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Joseph Butiku.

Alipendekeza ibara ya 4 (1) ya rasimu inayotambua lugha ya taifa kuwa Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ndiyo na pale anapokuja Kiongozi asiyefahamu lugha hiyo atafutwe mkalimani.

“Kiongozi anapokuwa ndani na nje ya nchi aongee kwa Kiswahili halafu atafutwe mkalimani awatafsirie hao viongozi kutoka mataifa mengine… hii ndiyo njia ya kukienzi Kiswahili”alisema.

Kwa upande wao, Benedict Kimolo kutoka Kata ya Pasua na Steven Ngassa kutoka Kata ya Kiusa, walipendekeza Kiswahili kitumike katika kuandika hukumu na uamuzi madogo mahakamani.

Ngassa alienda mbali zaidi na kupendekeza hata neno “Lugha ya Kiingereza” linaloonekana katika Ibara ya 4(2) ya Rasimu ya Katiba Mpya lisitamkwe kabisa kwenye katiba mpya.

“Lugha ya Kiingereza isitamkwe kabisa kwenye katiba hii bali Kiswahili tu kitumike hadi kwenye uandishi wa hukumu mahakamani kwani watanzania wengi hawajui Kiingereza”alisema.

Joseph Kisaka kutoka Kata ya Mfumuni alisema ni batili katika kutamka Tanzania Bara bila kuwapo mshirika mwingine wakati jina Tanzania lilitokana na muunganiko wa Tanganyika na Zanzibar.

Tangu kuanza kwa mchakato wa maoni ya katiba, wadau mbalimbali wamekuwa wakipendekeza Kiswahili kiingizwe kwenye katiba kuwa ni lugha ya taifa, mapendekezo ambayo hata hivyo bado hayajatekelezeka na kufanya kilio hicho kiendelee kusikika kwenye mijadala mbalimbali inayoendelea nchini.

Kiswahli kinajulikana kuwa ni lugha ya Taifa na ndiyo lugha inayotumika kufundishia shuleni na kuzungumzwa katika maeneo ya kazi.

Hata hivyo lugha hiyo ambayo ni tunu ya taifa haijatambuliwa rasmi kwenye katiba kuwa ni lugha ya taifa.

Chanzo: Mwananchi