KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imezindua huduma zake za simu kwa kutumia teknolojia ya 4G LTE Mkoani Tanga. Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigela alisema viongozi na wananchi wa mkoa huo wamefarijika sana na tukio la TTCL kuzinduwa huduma za 4G LTE katika Mkoa na kuahidi kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo.
“..Mimi na Watendaji wenzangu na Wananchi wa Mkoa wa Tanga kwa ujumla, tumefarijika sana kwa tukio hili la uzinduzi wa huduma za 4G LTE za Kampuni ya Kizalendo ya TTCL katika Mkoa wetu. Karibuni sana Mkoani Tanga,” alisema Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Shigela akizinduwa huduma hiyo.
Mkuu wa Mkoa alisema Tanga ni Jiji la kibiashara lenye shughuli nyingi za kiuchumi zinazogusa sekta nyingi, zikiwemoa elimu ngazi mbalimbali wakulima na wafanyabiashara, ikiwa ni makundi yenye idadi kubwa ya watu yanayohitaji sana Mawasiliano ya uhakika na nafuu katika kufanikisha shughuli zao.
“…Tanga ni Jiji la kibiashara lenye shughuli nyingi za kiuchumi zinazogusa sekta nyingi. Aidha Tanga ni kituo kikubwa cha Kitaaluma hapa nchini ikiwa na idadi kubwa ya shule na Tasisi za Elimu zinazotoa ujuzi wa ngazi mbalimbali. Katika jamii hii ya Mkoa wa Tanga yapo makundi yenye idadi kubwa ya watu kama vile Wanafunzi, Wafanyakazi wa Sekta mbali mbali, Wafanyabiashara na Wakulima ambao wote hawa, wanahitaji sana Mawasiliano ya uhakika na yenye tozo nafuu katika kufanikisha shughuli zao.” Alisema Shigela.
Aidha mkuu huyo wa mkoa aliongeza ya kwamba, TTCL ni Kampuni iliyopewa jukumu la kuwaunganisha Wananchi popote walipo kwa Mawasiliano ya uhakika huku ikibeba pia jukumu la kufanikisha utendaji wa Sekta nyingine zote zikiwemo shughuli za ulinzi na Usalama wa nchi.
Alisema wananchi wanataka kuiona kampuni hiyo ikitimiza ndoto ya Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye mara zote anataka kuona mashirika ya Umma yakiwa hai, yakijiendesha kwa faida na kuchangia Pato la Taifa na ukuaji wa Sekta nyingine na hivyo kufanikisha mpango mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuifanya Nchi yetu kuwa Nchi ya Uchumi wa kati, Nchi ya Uchumi wa Viwanda.
“…Natumia fursa hii kukuhakikishia kwamba, Tanga ni soko la uhakika la bidhaa na huduma za TTCL. Tunachohitaji ni huduma bora za uhakika wakati wote pamoja na huduma za gharama nafuu ambazo makundi yote katika jamii tutaweza kumudu,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba akizungumza awali kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa alisema TTCL inatekeleza Mpango Mkakati wa Biashara wa miaka mitatu (Strategic Business Plan 2016-2018) unaolenga kuboresha na kuleta huduma mpya katika soko, kuongeza tija na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa Wateja wetu hasa tukizingatia kuwa TTCL ni Mhimili Mkuu wa Mawasiliano nchini Tanzania.
Alisema hivi sasa TTCL ipo katika mpango kabambe wa kuboresha miundombinu ya mtandao wa Simu na Data, kuondoa mitambo chakavu, kusimika mitambo mipya ya kisasa ili kutoa huduma bora na zenye kukidhi mahitaji na kukabiliana na ushindani.
“…Hii ni TTCL mpya, yenye huduma bora za kabla na baada kwa Wateja, yenye huduma za uhakika wakati wote na mahali popote iwe ni nyumbani, sehemu za kazi, katika Sekta za Kilimo, Ufugaji na biashara, huduma za Jamii kama Afya, Elimu, na hata kwenye vyombo vya usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” alisema Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba.
Akifafanua zaidi alisema mawasiliano kwa mtandao wa 4G LTE unapatikana katika eneo lote la katikati ya Jiji pamoja na badhi ya maeneo ya nje ya Jiji kama vile Kange na Msambweni. Alisema ahadi ya TTCL kwa Wana Tanga ni kuhakikisha ndani ya kipindi kifupi kijacho, itasambaza huduma hizo katika maeneo mengine ya Mkoa na hatimaye kulifanya Jiji zima la Tanga kufurahia huduma za TTCL.
“…Ombi letu kwako Mhe Mkuu wa Mkoa, Watendaji wa Ofisi yako na Watanzania wote, tunaomba mtuamini na kutuunga mkono kwa kutumia huduma zetu. Kwa kutuunga mkono mtaiwezesha TTCL kuwahudumia Watanzania kikamilifu na kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya Nchi yetu.