KAMPUNI ya Simu Tanzania TTCL, imezindua Huduma za TTCL 4G LTE katika Jiji la Mwanza siku ya Jumatatu, Januari 23, 2017. Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe John Mongela alieongozana na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Mary Tesha Onesmo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamanda, Ahmed Msangi.
Uzinduzi huo unaifanya Mwanza kuwa miongoni mwa Mikoa ya awali kabisa kupata huduma za 4G LTE ya TTCL yenye kiwango cha juu kabisa cha Ubora, kasi na gharama nafuu kupita kiasi. Mikoa mingine ambayo tayari kampuni hiyo imepeleka huduma za 4G LTE ya TTCL ni pamoja na Dar Es Salaam, Dodoma, Arusha, Mbeya,Morogoro, Pwani na Zanzibar.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mh. John Mongera alisema TTCL ni kampuni Mama wa Mawasiliano nchini, iliyopewa jukumu la kuwaunganisha Wananchi popote walipo, inabeba jukumu la kufanikisha utendaji wa Sekta nyingine zote zikiwemo shughuli za ulinzi na Usalama wa nchi.
“Watanzania tunataka kuiona TTCL yetu ikichukua nafasi yake ya kuwa moja ya mashirika muhimu ya Umma yanayochangia Pato la Taifa na ukuaji wa sekta nyingine na hivyo kufanikisha mpango mkakati wa Nchi yetu kuwa Nchi ya Uchumi wa kati, Nchi ya Uchumi wa Viwanda,” alisema Mkuu wa Mkoa, Mh. John Mongera.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri W. Kindamba akizungumza katika uzinduzi huo aliwahakikishia Watanzania na wateja wetu wote wa ndani na nje ya Nchi kuwa, kwa juhudi hizi tunazochukua na kwa ushirikiano mkubwa tunaopata kutoka Serikalini na kwa Wadau wetu, TTCL itafanya mapinduzi makubwa na kwa hakika itarejea katika nafasi yake ya kuwa kinara wa utoaji huduma za Mawasiliano nchini Tanzania.
“TTCL 4G LTE MWANZA TUMEWAFIKIA”