Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imepinga madai yaliyotolewa na Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (TEWUTA) jana dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na kufafanua kuwa madai hayo si ya kweli zaidi ya upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi na kutaka kuikwamisha jitihada za TTCL katika maendeleo.
Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari leo Makao Makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam alisema madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL hayana ukweli wowote bali wahusika walilenga kuupotosha umma.
“Menejimenti ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), inapenda kuujulisha Umma kuwa, madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL si sahihi. Hoja hizo zimejikita katika upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha malengo binafsi ya wahusika na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye nia na malengo ya kutekeleza mpango mkakakti wa kuiboresha na kuiimarisha Kampuni ya Simu Tanzania.
Akifafanua zaidi Meneja Uhusiano huyo wa TTCL alisema mwaka 2007 Kampuni ya Simu Tanzania ilifanya mabadiliko ya Muundo wa Kampuni ili kuendana na hali ya soko la Ushindani katika sekta ya mawasiliano na Muundo uliopo sasa ni ule uliopitishwa na kuanza Kutumika mwaka 2007 baada ya kuidhinishwa na kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
Alisema menejimenti mpya ya TTCL iliyoanza kazi Februari 2013 iliainisha changamoto mbalimbali za kibiashara na kutengeneza Mpango Mkakati utakaoletab mabadiliko ya kibiashara na kuongeza tija, huku ikizingatia mabadiliko ya Kibiashara na ushindani wa soko katika sekta ya mawasiliano, Menejimenti iliomba na kupata kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta Mshauri mwelekezi kwa njia ya Zabuni ili kupitia na Kushauri juu ya Muundo Mpya wa Kampuni utakaoendana na Mahitaji ya Kibiashara na kuleta ufanisi.
Aliongeza kuwa matokeo ya Kazi ya Mshauri mwelekezi yamelenga kubadilisha muundo wa Kampuni, Muundo wa Mishahara na Muundo wa utumishi. Mpango huu wa Mabadiliko ya Kibiashara unategemewa kukamilika katika kipindi cha mwaka 2016. Aidha alifafanua kuwa muundo wa mishahara unaotumika hivi sasa ni ule uliopitishwa Mwaka 2007 baada ya Kubadilika kwa Muundo wa Kampuni kama ulivyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa TTCL.
“…Mfumo huu uliiweka TTCL katika nafasi ya kukabiliana na soko la ajira kimaslahi. Mfumo huu wa Mishahara ulizingatia pia matakwa ya kisheria ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6/2004 zimeainishwa aina tatu za Mikataba ya Ajira. Yaani: Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalumu (Unspecified period of time), Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum (Fixed Employment contracts) na pia Mkataba wa Ajira wa kazi Maalum (Special Task)…”
“…Hivyo Muundo wa Mishahara uliopitishwa mwaka 2007 uliainisha madaraja ya malipo na viwango husika ikiainisha aina ya mkabata, Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalum na Mkataba wa Ajira wa Muda Maalum. Katika muundo huu madaraja na ngazi za Mishahara zimegawanyika katika ngazi Kumi (10) kuanzia TTCL 1 (Ikiwa ndio Kiwango cha Juu) hadi TTCL 10 (Ikiwa ndio kiwango kidogo) Muundo huu uko wazi na ndio unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu Tanzania. Hakuna ulipaji wa mishahara (Payroll) yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa,” alifafanua Meneja Uhusiano huyo katika taarifa yake.
Akizungumzia kuhusu Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL alisema imekuwa na mchango mkubwa katika kusukuma maendeleo ya TTCL chini ya uenyekiti wa Dk. Enos Bukuku na baadae chini ya Mwenyekiti wa muda Jaji Joseph Sinde Warioba.
Aliyataja baadhi ya mambo mengi yaliofanywa na Bodi hiyo kuwa ni pamoja na kuondoka kwa Mbia Mwenza Bharti Airtel na pia kuishauri Serikali juu ya umuhimu wa kuondoka kwa Bharti Airtel ndani ya TTCL ili kuwezesha juhudi za dhati za kuifufua TTCL.
“..Bodi imetoa ushauri, miongozo na maelekezo kwa menejimenti, imeshiriki vikao vya majadiliano ya kuondoka kwa Bharti Airtel na kipekee, imefanya mawasiliano na ofisi za Serikali zikiwepo Ofisi ya Rais na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kusisitiza umuhimu wa Kuondoka kwa Bharti Airtel. Juhudi hizi zimechangia sana kusukuma swala hili ambalo kwa sasa liko katika hatua za mwisho…,” alisema Bwana Mushi.
Bodi ya wakurugenzi ilipitisha uamuzi wa TTCL kuingia katika mradi ya mabadiliko wa mfumo wa kibiashara ili TTCL iweze kupanua mtandao wake na kuwa wa kisasa zaidi kuweza kutoa huduma mbalimbali kwa teknolojia ya kisasa (GSM, UMTS & LTE) zikiwemo huduma za simu za mkononi na mawasiliano ya data kwa ufanisi zaidi ili Kampuni iweze kukabiliana na ushindani ulioko sokoni na kuongeza pato lake. Tayari sehemu ya mradi huo imekamilika (4G LTE) ya kutoa huduma ya data kwa kiwango cha juu katika sehemu ya maeneo kadhaa ya Dar es Salaam. Utekelezaji wa mradi utaendelea kwa sehemu zingine.
Kwa kushirikiana na Serikali Bodi inaendelea kutoa ushirikiano stahiki katika hatua za kuiboresha TTCL zikiwemo kuhakikisha TTCL inapata mtaji wa kutosha kuendesha shughuli za mawasiliano ndani na nje ya nchi kuweza kuendana na Sera za Taifa na kuboresha pato la Kampuni. Bodi imekua ikitoa mchango mkubwa kuhakikiksha Mkongo wa Taifa unaendeshwa vizuri kwa kuwa na mawasiliano wakati wote. Aidha, sambamba na maamuzi ya Baraza la Mawaziri juu ya TTCL kumilikishwa Mkongo wa Taifa, Bodi ya Wakurugezi imetoa mchango mkubwa juu ya ufuatiliaji wa swala hili kwenye Wizara husika. Serikali kupitia wizara hya Mawasiliano iko katika hatua nzuri katika kukamilisha swala hili.” Alieleza katika taarifa yake.
Akizungumzia Kampuni ya Rubiem ambaye ni Mshauri mwelekezi aliyepatikana kwa kufuata taratibu sahihi za manunuzi ya Umma, alisema mchango wa kampuni hiyo katika mpango wa mageuzi kibiashara ni mkubwa na unaonekana dhahiri tofauti na madai yaliyotolewa.
“…Matokeo ya kazi yake yataanza kuonekana mwishoni mwa mwaka huu ambapo huduma na bidhaa mpya zitaingia sokoni. Mshauri huyu anatarajia kukamilisha kazi yake katika robo ya kwanza ya mwaka 2016. Ieleweke pia kwamba, hatua ya Menejimenti kumuongezea muda mshauri huyu hazihusishi gharama zozote za nyongeza nje ya mkataba wake wa kazi na TTCL.
Menejimenti ya Kampuniya Simu Tanzania TTCL inaomba kutumia fursa hii kuwajulisha Umma kwamba, hali ya Kampuni yao ni thabiti, utendaji wa kazi unaendelea vizuri na jitihada mbali mbali za kuboresha huduma zinaendelea kwa ufanisi mkubwa,” alifafanua Bwana Mushi kwa wanahabari.
“…Menejimenti ya Kampuniya Simu Tanzania TTCL inapenda kuujulisha Umma kuwa, oja zote zilizotolewa na TEWUTA si za kweli, ni taarifa zilizopotoshwa kwa makusudi, zikilenga kufanikisha malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Sayansi na Mawasiliano, Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye lengo la kuifanya Kampuni kutimiza kikamilifu Wajibu wake kwa Umma. Ieleweke pia kwamba, Muundo wa mishahara ya Watumishi wa Kampuni ya simuTanzania TTCL uko wazi na ndio unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni ya Simu Tanzania. Ofisi inayolipa mishahara ya wafanyakazi wote wa TTCL iko idara ya Fedha na kusimamiwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Simu. Hakuna Payroll yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa, hakuna posho zozote zinalipwa kinyume na utaratibu.” alieleza Meneja huyo wa TTCL.