Na Mwandishi Wetu, Kagera
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL), imekabidhi msaada wa tani 30 za mifuko ya saruji zenye thamani ya shilingi milioni kumi ili kusaidia jitihada za Serikali za kukarabati miundombinu mbalimbali iliyoathirika na tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni mkoani Kagera.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema kampuni hiyo imeguswa na tukio zima lililowapata wananchi wa mkoa huo hivyo kuungana na wadau wengine kusaidia.
Dk. Kazaura alisema licha ya msaada huo, TTCL imekuwa ikiimarisha huduma za mawasiliano mkoani Kagera kukabiliana na maafa yaliyosababishwa na Tetemeko la ardhi lilitokea tarehe 10 Septemba mwaka huu. Alisema TTCL imeongeza timu ya wafanyakazi wake Kitengo cha Ufundi kukabiliana na athari za tukio hilo kwa Wateja wake pamoja na kusaidia jitihada za Serikali na kukabiliana na janga hilo kwa kutoa taarifa za mara kwa mara kutoka maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Kagera na kufanikisha uratibu na upokeaji wa misaada stahiki kwa waathirika.
Alisema, licha ya tukio hilo kuathiri wafanyakazi na Miundo mbinu ya Kampuni hiyo, TTCL imejiwekea lengo la kuhakikisha kuwa huduma za Mawasiliano zinaendelea kuwa za uhakika na kiwango cha juu kabisa cha ubora kwa Wateja wake sambamba na kuwawezesha watoa huduma wengine wanaohudumiwa na TTCL kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wanatoa huduma zao kwa ufanisi wakati wote.
Dk. Kazaura ameongeza kuwa, TTCL imetoa huduma ya Mawasiliano yasiyolipiwa kwa Ofisi za Wakuu wa Wilaya za Misenyi, Karagwe na Bukoba Mjini ili kufanikisha zoezi la kukusanya taarifa, kupokea misaada kwa waathirika na kuwezesha shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii kwa Wananchi wa Mkoa wa Kagera na nchi jirani kuendelea kama kawaida.
Akishukuru kwa msaada huo wa TTCL, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu alisema mchango huo ni mkubwa sana kwa kuwa wakati wote tangu kutokea kwa tukio hilo kwani huduma za Mawasiliano zimekuwa za uhakika wakati wote na pale palipoathirika, TTCL imechukua hatua za haraka za kurekebisha athari hizo.
“Ninawashukuru sana TTCL, kwa kweli mmetimiza Wajibu wenu na ninaona fahari kubwa kwa Shirika la Umma kufanya kazi hii kwa juhudi kubwa na moyo wa kujitoa kwa dhati kiasi hiki. Msaada wenu wa Mawasiliano umesaidia sana nchi nzima kufahamu yanayoendelea Mkoani Kagera, Watanzania popote walipo wanawasiliana, wanasaidiana na kupeana moyo katika kipindi hiki kigumu, hii ni kutokana na juhudi zenu na huduma zenu nzuri. Napenda kuwashukuru sana na kuwahakikishia kuwa, msaada wenu utatumika vyema kuleta ahueni kwa Watanzania wenzetu walioathirika,” alisema Meja Jenerali Mstaafu Salim Mustafa Kijuu.
Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kutoa wito kwa Taasisi nyingine za Umma na binafsi kuiga mfano wa TTCL kwa kusaidia waathirika wa tukio hilo kutokana tathmini za madhara ya tukio hili kuonesha athari kubwa kwa maisha ya Wananchi na miundo mbinu mbali mbali.