Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imekabidhi mradi wa kuiunganisha matawi 12 ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) katika huduma za mawasiliano ya sauti, intaneti pamoja na data ili kuviwezesha vituo hivyo kufanya kazi katika mfumo wa kisasa kimawasiliano jambo ambalo litaboresha utendaji kazi wa kampuni hiyo.
Akikabidhi mradi huo leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Mkuu wa Masoko na Mauzo wa kampuni ya TTCL, Peter Ngota alisema kwa sasa wamekamilisha kuyaunga kimawasiliano ya kisasa matawi 12 ya kampuni ya bia Tanzania ambayo ni pamoja na tawi kuu la Dar es salaam (HQ), Arusha, Moshi, Mwanza, Ubungo, Mwenge, Konyagi, Masaki, Bukoba, Shinyanga, Iringa na tawi la Tanga.
Alisema mfumo huo wa mawasiliano unaunganisha makao makuu ya ofisi na matawi yake ambayo yako maeneo tofauti nchini kwa lengo la kurahisisha utoaji na upokeaji wa Taarifa
(Data) huku ukiwa salama tofauti na mifumo mingine.
“…Katika mfumo huu wa Multiprotocol Label Switching Virtual Private Network (MPLS VPN), Tanzania Breweries Ltd inapata huduma ya sauti, intaneti pamoja na data. Kwa huduma hizi TBL sasa iendelee kwa kasi kuboresha mifumo ambayo itasaidia kuongeza tija katika utendaji kazi wake na kwa wateja kwa ujumla,” alisema Ngota.
Ofisa huyo Mkuu wa Masoko na Mauzo aliongeza kuwa kwa sasa TTCL ni kampuni pekee yenye mtandao wa Mkongo (Fibre) ambao umesambaa nchi nzima huku ukiwa chachu ya kuleta mabadiliko katika kutoa huduma kwa wananchi na utendaji kazi wa jumla wa makampuni mbalimbali.
TTCL imekuwa nguzo muhimu kwa Taasisi za kifedha (Kibenki), Balozi, Mashirika, Wizara na taasisi za serikali, makampuni ya kimataifa na binafsi katika kuboresha utendaji na uendeshaji wa shughuli zao kisayansi na kukidhi viwango vya kimataifa. TTCL pia imefanikiwa kuunganisha wateja mbalimbali ikiwa ni pamoja taasisi na ofisi za serikali; TAMISEMI, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Wizara ya Fedha, Kampuniya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Alisema huduma hiyo ya mkongo pia imerahisisha kazi katika Hospitali ya Muhimbili, Mwananyamala, Temeke, MOI, Bugando, KCMC pamoja na Hospitali za Mkoa nchi nzima ikiwemo Zanzibar pia zinaendelea kuunganishwa kupitia Mkongo wa TTCL kwa huduma bora za kiafya kupitia afya mtandao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni ya TBL, Kevin O’Flaherty akipokea mradi huo alisema tayari wameanza kuona mafanikio makubwa baada ya kuanza kutumia mfumo huo huku ukisaidia kukua kwa biashara yao tofauti na awali.
Aidha alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kukua kila uchao kampuni hazina budi kufanya kazi kwa kutumia teknolojia mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa kazi na ubora hali itakayochangia kukua pia kwa biashara zao. “…Tayari tumeanza kuona mafanikio tangu kuanza kutumia huduma hii na tunaamini tutapata mafanikio zaidi, kwa sasa unaweza kutofautisha na ilivyokuwa kabla ya kuanza kutumia MPLS VPN,” alisema O’Flaherty.