KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) leo imezinduwa kituo kipya cha huduma kwa wateja kilichopo katika Jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam, kituo kitakacho toa huduma kwa wateja mbalimbali wa kampuni hiyo pamoja na wananchi wengine wanaoitaji huduma za TTCL.
Akizinduwa kituo hicho, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba alisema uzinduzi huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka 2016, ikiwa na lengo la kutambua mchango wa wateja kutumia huduma za kampuni hiyo na kuchangia maendeleo ya kampuni hiyo na taifa kwa ujumla.
Kindamba alisema uzinduzi wa kicho hicho cha huduma kwa wateja hasa wa eneo la Ubungo ni sehemu ya mpango wa TTCL katika kuboresha vituo na maduka yake nchi nzima ili yaweze kutoa huduma bora na kwa ufanisi zaidi. Alisema kutokana na mahitaji ya wateja, TTCL imedhamiria kuongeza idadi ya vituo hivyo pamoja na maduka yake ikiwa ni mpango wa kusogeza zaidi huduma kwa wateja maeneo anuai.
“Kituo hiki cha huduma kwa wateja cha Ubungo ambacho kinazinduliwa leo, kitahudumia wateja kutoka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Eneo hili la Ubungo ni lango la kuingia katikati ya jiji huku maeneo yanayozunguka yakiwa na idadi kubwa ya watu, hivyo tunategemea kupata wateja wengi wanaoingia jijini Dar es Salaam pamoja na wanaoishi maeneo ya jirani ikiwemo Sinza na Mabibo..,” alisema.
Aidha aliongeza kuwa kutokana na maboresho makubwa ambayo kampuni hiyo ya kizalendo imeyafanya imejipanga kufanya kazi kwa ufanisi na kutekeleza falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu, huku ikitumia rasilimali za nchi vizuri na kuchangia mageuzi yanayoendelea nchini ya kuifanya Tanzania kupiga hatua kuelekea nchi ya uchumi wa kati na nchi ya viwanda.
Kituo hicho kipya kitatoa huduma mbalimbali zikiwemo kuunganisha wateja wa huduma za intaneti, kurejesha namba iliyopotea, kufanya malipo ya ankara za huduma za TTCL, kusajili namba za simu za 4G, kuuza muda wa maongezi, kuuza modemu zenye ofa kabambe, kupata Routers na kuunganishwa na huduma za T-TV inayowezesha wateja kutazama matangazo ya vituo vya luninga moja kwa moja kupitia simu zao za mkononi na vifaa vingine vya kisasa vya mawasiliano.