KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) sasa inayawezesha wateja wake ikiwa ni pamoja na kampuni, taasisi na ofisi za Serikali kupata mawasiliano ya intaneti sehemu ambazo ziko mbali na njia ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa njia ya Satelaiti.
Akizungumza katika Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa, katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Sabasaba, Ofisa Mtatuzi wa Masuala ya Kiufundi wa TTCL, Fredrick Benard alisema teknolojia hiyo mpya ni muhimu sana kwa makapuni na wateja wengine kwani ina ubora, uhakika kwa matumizi na ni bei nafuu.
Alisema mbali na mawasiliano ya intaneti wateja wanaweza pia kupata huduma ya kuunganishwa kimawasiliano ya shughuli za kiofisi kwa ofisi zaidi ya mbili ambazo zipo maeneo tofauti na kushirikiana kwa taarifa na mifumo ya kikomyuta (Mpls Vpn).
Alisema TTCL iliamua kuleta huduma hiyo kutokana na mahitaji makubwa ya matumizi ya intaneti kwa shughuli za maendeleo. “Kuna maeneo ambayo awali yalihitaji huduma ya Mkongo(Fibre) lakini kutokana na umbali pamoja na gharama imekuwa ngumu kuwapelekea huduma, suluhisho la changamoto hiyo imeishapatikana, sasa taasisi hizo zinaweza pata mawasiliano ya intaneti kwa njia ya Satelaiti, ubora wake ni ule ule kama unaopatikana kwenye Mkongo (Fibre), Benard.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Biashara Kanda ya Dar es salaam, Karim Bablia akifafanua zaidi juu ya huduma hiyo alisema itawasaidia zaidi wamiliki wa hoteli za kitalii, hospitali, vyuo na shule ambazo awali zilihitaji huduma ya intaneti yenye kasi maeneo yasio na mkongo na kupata huduma hiyo na kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo yao.
“…Kinachotakiwa mteja anatakiwa kuleta maombi rasmi ya huduma anayoitaka kama ni internet au Mpls Vpn baada ya hapo mteja atapelekewa tathmini ya gharama ya kuunganishiwa juu ya huduma hiyo,” alisema.
Aidha Bablia aliongeza kuwa teknolojia ya satelaiti itaweza kutoa huduma za intaneti kwa wateja wake walio nje ya uwezo wa kufikiwa na huduma ya intaneti kupitia waya (Mkongo). Hivyo basi, teknolojia hii itashughulikia haraka changamoto za TEHAMA nchini, na kuchangia katika upatikanaji wa huduma na taarifa kwa haraka zaidi.
“Kupitia Satelaiti wateja wanategema kupata huduma mbalimbali kama vile intaneti yenye kasi, Mkutano kwa njia ya video (Video conference) na MPLS VPN,” alifafanua.
Alibainisha kuwa kampuni ya Simu Tanzania(TTCL) sasa inaendelea na mkakati wake kufanya mabadiliko katika kampuni na biashara kwa lengo la kuhakikisha kuwa inatoa fursa kwa taasisi, makampuni ya umma na binafsi ili waweze kuongeza ufanisi na uzalisha katika maeneo yao, kuongeza pato na kukuza uchumi wa Taifa.