Na Mwandishi Wetu,
TANZANIA inafanya mazungumzo na mataifa anuai ya Afrika zikiwemo nchini za Angola, Namibia pamoja na Zambia ili kuweza kuunganisha mkongo wa taifa na mikongo kutoka mataifa mengine ili iweze kupata huduma kwenye mikongo ya baharini iliyoko pwani ya Bahari ya Atlantiki lengo ikiwa ni kusaidia kupatikana kwa huduma hiyo katika nchi za katikati mwa Bara la Afrika.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Dk. Kamugisha Kazaura alipokuwa akizungumza katika Mkutano wa kimataifa wa ‘Connect 2 Connect’ unaoshirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya mawasiliano barani Afrika, viongozi wa serikali wa mataifa mbalimbali ya africa, pamoja na taasisi binafsi zinazotoa huduma za mawasiliano na zile zinazo tengeneza vifaa vya mawasiliano.
Mkutano huo ambao unafanyika jijini Dar es Salaa ikiwa ni mara ya tatu kufanyika Tanzania umeanza leo Julai 28 na utamalizika Julai 29, 2015 huku ukijadili uboreshaji wa masuala anuai ya mawasiliano na changamoto kwa Bara la Afrika na namna sekta hiyo inavyoweza kutumika kuendeleza mataifa husika.
“…Kwa Tanzania tuna bahati kwamba tumejenga mkongo wetu ambao mafanikio yake ni mengi kwa sasa, na mfano tunafanya mazungumzo na Zambia, Angola na Namibia kuweza kuunganisha mkongo wa mataifa yetu kwenda kupata huduma kwenye mikongo ya baharini iliyoko pwani ya bahari ya Atlantiki hii itasaidia kupata huduma bora zaidi na nafuu,” alisema Dk. Kamugisha Kazaura.
Alisema makubaliano ya kunganisha mikongo hii ya taifa kwa nchi mbalimbali kwenye mikongo ya baharini, kwa nchi za Pwani ya Afrika Mashariki na kuunganisha pia katika mikongo ambayo ipo Pwani ya Magharibi ya Afrika kwenye bahari ya Atlantiki itasaidia huduma hiyo kufikia katika nchi za katikati mwa Bara la Afrika hatimaye nazo kunufaika na mawasiliano hayo.
Aidha kifafanua zaidi, alisema nchini Tanzania faida ya mkongo kwa sasa kila mtu anaweza kushuhudia kutokana na kupungua kwa gharama za simu na intaneti tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma. “…Asilimia 90 ya gharama za simu na intaneti zimepungua, na kundi kubwa limenufaika hata nje ya nchi, kabla ya mkongo bei ya kupiga simu ilikuwa juu lakini sasa imeshuka,” alisema.
Hata hivyo alisema mataifa ya nje pia ikiwemo Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi, Malawi, Uganda na zamani yamenufaika pia na mkongo wa Tanzania. Mkutano huo wa Connect 2 Connect mwaka huu unakauli mbiu ya kuiunganisha mikongo ya Bara la Afrika pwani kwa pwani yaani ‘Connecting Africa Coast to Coast’.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Selina M. Lyimo alisema alisema mkutano huo uliojumuisha mataifa mengi kutoka Afrika na ambao utagusia pia kuhusiana na masuala ya kutumia teknolojia hiyo ya Mawasiliano ili kuwezesha nchi hizo kuingia katika teknolojia bora zaidi na kuitumia teknolojia hiyo iweze kuleta maendeleo ya kiuchumi.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com