KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) leo imetoa msaada wa vyakula na bidhaa mbalimbali kwa Hospitali ya Wagonjwa wa Kansa Ocean Road ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni kuwasaidia wagonjwa hao kusherehekea Siku Kuu ya Chrismas pamoja na Mwaka Mpya. Misaada hiyo ni sehemu ya kampuni ya TTCL kuamua kushirikiana na jamii katika maeneo mbalimbali ikiwa ni ishara ya kurejesha sehemu ya faida yao ya kampuni kwa jamii hasa iliyo katika wakati mgumu.
Akikabidhi msaada huo wa unga, mafuta ya kula, sukari, chumvi na maji ya kunywa, ambayo kwa pamoja vinagharimu shilingi milioni tatu (3), Mkuu wa Huduma kwa wateja wa kampuni ya TTCL, Laibu Leonard alisema tukio hilo ni utaratibu wa kampuni yao hasa nyakati za sikukuu ambapo uwafariji wateja wao waliopo katika mazingira ya uhitaji msaada kwa chochote.
Alisema Hospitali hiyo ya Wagonjwa wa Kansa, Ocean Road ipo mbioni kufungwa mkongo wa mawasiliano unaosimamiwa na TTCL ili kuwafanya madaktari hospitali hiyo kuweza kutoa huduma kwa njia ya mawasiliano ya picha hata kwa mgonjwa ambaye yupo mikoani. Alisema tayari maandalizi ya awali yamefanywa kati ya TTCL na hospitali hiyo hivyo mwakani huduma ya matibabu kwa njia ya mtandao kwa kutumia mkongo wa mawasiliano itaanza kutolewa na madaktari.
Akizungumzia manufaa ya huduma hiyo, Leonard alisema huduma hiyo ya matibabu ya picha kwa mawasiliano inapunguza gharama za matibabu kwa kiasi kikubwa kwani daktari aliye nje ya nchi kama India anaweza kumtibu mgonjwa aliyelazwa hospitali za Tanzania bila kikwazo. “…Tumeleta msaada huu kwa kuwa hawa ni miongoni mwa wadau wetu kibiashara, sasa hivi tunamalizia utaratibu wa wao kutumia mkongo wetu kwa ajili ya shughuli za matibabu…ambayo kwa kiasi kikubwa yanapunguza gharama sana, badala ya mgonjwa asafiri kwenda nje ya nchi kufuata huduma anaweza kutibiwa akiwa hapahapa kwa kutumia matibabu ya picha kutumia mtandao,” alisema.
Akipokea msaada huo, Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Ocean Road, Marry Haule alisema wamefarijika na msaada uliotolewa na TTCL kwani msaada waliouleta ni sehemu ya matibabu kwa wagonjwa wao na kuhaidi kuutumia kama ilivyo kusudiwa. Alisema wagonjwa wa kansa wanahimizwa kula sembe ili iweze kuwasaidia kama sehemu ya matibabu jambo ambalo TTCL imelifanya, hivyo kuwapongeza na kuomba kampuni zingine zifuate mfano wa kampuni hiyo kwa kuwakumbuka wagonjwa.
Huduma ya matibabu kwa njia ya mtandao (picha) inayowezeshwa na mawasiliano ya mkongo wa mawasiliano wa taifa, imesha anza kazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya KCMC, Hospitali ya Tumbi Kibaha, pamoja na Hospitali za Mwananyamala na Temeke zote za jijini Dar es Salaam.