TTCL Mkoani Mbeya Waisaidia Sekondari ya Luswisi

 Mbunge Aliko Kibona pamoja na Meneja wa TTCL wakikabidhiana mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.

Mbunge Aliko Kibona pamoja na Meneja wa TTCL wakikabidhiana mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu.

 Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, James Mlaguzi akisoma taarifa ya msaada uliotolewa na kampuni hiyo katika shule ya Sekondari Luswisi.
 Mbunge wa Ileje aliyemaliza muda wake, Aliko Kibona akitoa shukrani kwa niaba ya  wananchi wa Kata ya Luswisi kwa kampuni ya TTCL kutokana na msaada waliopokea.
 Mbunge na Meneja wakipongezana baada ya kukabidhiana Saruji na Mbao.
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Luswisi wakifurahia msaada uliotolewa na TTCL.
 Wanafunzi wakisaidia kushusha mifuko ya saruji iliyotolewa na kampuni ya TTCL.
 Watumishi wa TTCL Mbeya wakijadiliana jambo kabla ya kuanza makabidhiano ya msaada wa saruji na mbao katika shule ya sekondari Luswisi.
 Baadhi ya wanakijiji waliojitokeza kupokea msaada huo.
 Watumishi wa TTCL Mbeya wakimsikiliza Mbunge alipokuwa akitoa shukrani kwa  niaba ya wananchi.
  Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Luswisi, Mseven Ndangalaakielezea furaha yake baada ya kupokea msaada wa saruji na mbao kutoka TTCL.
 Ngoma za asili zikiendelea kutoa burudani katika hafla ya kukabidhiana msaada wa saruji na Mbao. 
*************
KAMPUNI ya simu ya TTCL imetoa
msaada wa saruji na mbao katika Shule ya Sekondari ya Luswisi iliyopo Kata ya
Luswisi Wilaya ya Ileje mkoani Mbeya kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za
Walimu na chumba kimoja cha darasa.
Kampuni hiyo ilitoa msaada wa
mifuko 100 ya saruji na mbao vyenye thamani ya shilingi Milioni tatu ikiwa ni
kupunguza changamoto inayowakabili Walimu wa Shule hiyo ambayo inawalimu 22
huku ikiwa na Nyumba moja iliyokamilika ambayo anaishi Mkuu wa Shule.
Wakizungumza baada ya kupokea
msaada huo baadhi ya Walimu hao wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Shule, Mseven
Ndangala, alisema Walimu wanaishi katika wakati mgumu kwani asilimia kubwa
wamepangishwa na wanakijiji sehemu ambayo ni mbali na eneo la shule.
Alisema Walimu wengi wamepanga
umbali wa kilomita 7 kutoka shuleni hivyo hulazimika kukodi pikipiki kuwapeleka
na kuwarudisha shule kwa gharama ya shilingi 6000 kwa siku hali inayowarudisha
kwenye umaskini na kupunguza ari ya kufundisha kutokana na kutumia gharama
kubwa kwenye usafiri.
Aliongeza kuwa hivi sasa kuna
walimu wapya watano ambao kwa mazingira yalivyo hawataweza kupanga kutokana na
ukosefu wa fedha na kuwalazimu kuishi walimu wote watano kwenye chumba kimoja
hali inayoonesha kuwakatisha tama kuendelea kufundisha shuleni hapo.
Awali akikabidhi msaada huo,
Meneja wa TTCL Mkoa wa Mbeya, James Mlaguzi, alisema Kampuni ilipata maombi
kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Ileje, Aliko Kibona kwa ajili ya kusaidia
kupunguza adha hiyo jambo ambalo lilikubaliwa na hatimaye kuwafikishia.
Alisema kampuni imejipanga
kuhakikisha mwishoni mwa mwaka huu inapeleka huduma za mawasiliano vijijini ili
kuwawezesha wakulima kutafuta masoko ya mazao yao kwa njia za mtandao.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo
la Ileje aliyemaliza muda wake, Aliko Kibona aliwashukuru kampuni ya TTCL
Hususani Afisa mtendaji Mkuu Dk. Kazaula Kamugisha kwa kumkubalia ombi lake ili
kuhakikisha walimu wanakuwa na mazingira mazuri ya kufundishia kwa kuwajengea
nyumba nzuri.
Aidha alitoa wito kwa Watendaji
wa vijijini na Kata kuhakikisha wanasimamia vizuri msaada huo kwa kuhakikisha
unafanya kazi zilizokusudiwa ili kuwaridhisha waliotoa misaada na hivyo
kuwafanya wawe na moyo wa kujitolea katika kipindi kingine.
Aliongeza kuwa ni wajibu wa
Wabunge, wadau na wananchi kuhakikisha wanatumia kila njia wanatengeneza
mazingira mazuri ya Walimu kuwa na ari kubwa ya kufundisha kuliko kuitegemea
Serikali kwa kila kitu.