WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Kampuni ya Simu Tanzania TTCL zimetiliana saini Mkataba wa huduma za Intaneti ambapo TTCL itaunganisha ofisi za Wakala hiyo nchi nzima kwa kutumia Mkongo wake wa Mawasiliano.
Hafla ya kutiliana saini makubaliano hayo imefanyika leo katika ofisi za Makao Makuu ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kuhudhuriwa na Mtendaji Mkuu (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, Afisa Mtendaji Mkuu (TTCL), Dkt Kamugisha Kazaura pamoja na maafisa Waandamizi kutoka TTCL na TANROADS.
Mradi huo utakaotekelezwa katika Mikoa 25 na Vituo (3) vya mizani utatumia miundombinu ya mawasiliano ya Kampuni ya TTCL iliyounganishwa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB). Mikoa hiyo ni pamoja Makao Makuu ya TANROADS, Mikoa ya Singida, Tabora, Kigoma, Tanga, Mtwara, Kibaha, Iringa, Musoma na Bukoba.
Mikoa mingine ni Dar es salaam(Keko na Mabibo), Lindi, Makambako, Mwanza, Songea, Manyara, Shinyanga, Dodoma, Mbeya, Sumbawanga, Simiyu(Bariadi), Arusha, Mpanda, Moshi, Geita na Morogoro
Kampuni ya Simu Tanzania TTCL inatekeleza Mpango Mkubwa wa Mageuzi ya Kibiashara ambao umelenga kuboresha miundombinu ya Mtandao na biashara ili kukidhi mahitaji ya wateja na Nchi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasilaino. Hadi sasa, Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) imeunganisha makampuni binafsi, Mashirika ya Umma na ofisi za serikali zaidi ya 80 kwenye miundombinu ya mawasiliano ya TTCL yenye ufanisi mkubwa wa kimawasiliano ndani na nje ya nchi.