Donald Trump amesema atafurusha wakimbizi kutoka Syria walio nchini Marekani iwapo atakuwa rais.
Bilionea huyo, ambaye kwa sasa anaongoza kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya kuwania urais kupitia chama cha Republican amesema katika mkutano wa kisiasa New Hampshire: “Nikishinda, watarudi kwao.”
Matamshi hayo ni tofauti na aliyoyatoa mapema mwezi huu akihojiwa na Fox News aliposema Marekani inafaa kuwapokea wakimbizi zaidi.
Mzozo wa wahamiaji umekuwa ukitatiza bara na Ulaya na Marekani imeahidi kupokea wakimbizi 10,000 kutoka Syria mwaka ujao.
Jumatano usiku, Bw Trump hadhira katika shule ya upili ya Keene: “Nasikia tunataka kupokea Wasyria 200,000. Na huenda wakawa – sikizeni, huenda wakawa wanachama wa Islamic State.”
Huku akiwataja kama “jeshi la watu 200,000”, baadaye aliongeza: “Ninawaonya watu wanaokuja hapa Syria kwamba nikishinda, nikishinda, watarudi kwao.
Trump anaongoza kwenye kura za maoni New Hampshire.
Awali alikosolewa sana baada ya kusema wahamiaji kutoka Mexico “wanaleta dawa za kulevya, uhalifu, na wabakaji”.
Trump alimlaumu Rais Barack Obama kwa mzozo huo ulioko Syria akisema: “Huko ni jehanamu Syria. Wanaishi jehanamu.”
Marekani imewapokea Wasyria 1,500 tangu kuanza kwa vita nchini humo miaka mine iliyopita.
Wanasiasa kadha wa chama cha Democrats wanaopania kuwania urais, akiwemo Hillary Clinton, wametoa wito kwa Marekani kuongeza idadi ya Wasyria kutoka 10,000 hadi 65,000.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani John Kerry ameahidi kupokea wakimbizi Zaidi kutoka maeneo mbalimbali duniani, akiongeza idadi ya wahamiaji wanaopokelewa kila mwaka kutoka 70,000 hadi 85,000 mwaka ujao na baadaye hadi 100,000 mwaka 2017.
-BBC