KUTOKANA na mgao wa umeme unaoendelea hivi sasa, Wizara ya nishati imechukua uamuzi wa kuhamisha transifoma
kutoka Chalinze ili ije itumike jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupunguza makali ya mgao wa umeme.
Tayari wizara hiyo imeshaagiza wakandarasi wa shirika la umeme kuhamisha transfoma hiyo ije jijini Dar es Salaam ifungwe katika kituo cha Kipawa na iwashwe kwa madhumuni ya kupunguza makali ya mgao wa umeme.
Wizara hiyo imetoa siku nane shughuli za ufungaji transofoma hiyo umalizike.
Transfoma hiyo imechukuliwa kutoka Chalinze ilikuwa ni ya mradi mwingine wa kuboresha umeme katika mikoa ya Pwani,Tanga, Mwanza na Shinyanga.
Bw. Abdulah Feresh, Meneja Mwandamizi wa Udhibiti Mifumo na Njia Kuu za Umeme alisema kwa muda huo uliotolewa wataweza kumaliza kazi hiyo kwa kuwa watahakikisha wanafanya kazi kwa saa 24 kila siku.