TRA Yapigilia Msumari Mgomo wa Wafanyabiashara Juu ya EFDs

Baadhi ya waduka yakiwa yamefungwa maeneo mbalimbali ya Kariakoo ikiwa ni kupinga matumizi ya mashine za kisasa za kukokotoa kodi, EFD.

Baadhi ya waduka yakiwa yamefungwa maeneo mbalimbali ya Kariakoo ikiwa ni kupinga matumizi ya mashine za kisasa za kukokotoa kodi, EFD.

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema matumizi ya mashine maalumu za kukokotoa kodi (EFDs) ni ya lazima na yapo kwa mujibu wa sheria za nchi hivyo kila wafanyabiashara anayehusika anapaswa kutumia kama ilivyoelekeza. Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA kwa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya mgomo wa baadhi ya wafanyabiashara maeneo mbalimbali ya nchi kufunga maduka wakigomea matumizi ya mashine za EFDS.

Katika taarifa hiyo TRA imeelezea kusikitishwa na kitendo cha wafanyabiashara kufunga maduka maeneo mbalimbali nchini, huku wengine wakiwalazimisha wenzao kufunga maduka kwa kuwatishia na kuwashurutisha.

“…Mamlaka ya Mapato Tanzania inapenda kuwafahamisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla kuwa watu wanaolazimisha wafanyabishara wenzao kufunga maduka kwa kuwatishia na kuwashurutisha wanavunja sheria kwa kusababisha uvunjifu wa amani nchini na hivyo mkono wa sheria utawafikia,” ilisema taarifa hiyo.
 
“…Ifahamike kuwa Matumizi ya mashine ya EFD ni jambo la kisheria na lilipitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2011. Pamoja na sheria kupitishwa, viongozi wakuu wa nchi walikwisha litolea tamko kwa nyakati tofauti kwa kuanzia na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mwezi wa Machi 2011,” ilieleza taarifa ya TRA juu ya mgomo huo.
 
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ili kuonesha msimamo wa serikali viongozi mbalimbali wa nchi akiwemo Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Billal aliwahi kusisitiza jambo hili Novemba 8, 2013 na pia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokuwa Desemba 2013.

Tarehe 29 Januari 2014, Waziri wa Fedha Mhe Saada Mkuya Salum aliweka bayana msimamo wa Serikali kwa kusisitiza kuwa Matumizi ya mashine za EFD ni swala la kisheria na litaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa sheria akisisitiza kuwa muda wa mwisho wa nyongeza kwa wafanyabishara kununua mashine ilikuwa ni Tarehe 31 Januari 2014 baada ya kuongeza muda mara tatu kwa nyakati tofuati.
 
“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pia kwa nyakati tofauti na maeneo tofuati imelitolea tamko jambo hili na itaendelea kufanya hivyo. Kwa masuala ya kiutendaji yaliyolalamikiwa yamefanyiwa kazi na yanaendelea kufanyiwa kazi ikiwemo utoaji wa Elimu kwa umma.”
 
“Mamlaka ya Mapato Tanzania inapenda kuwafahamisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla kuwa watu wanaolazimisha wafanyabishara wenzao kufunga maduka kwa kuwatishia na kuwashurutisha wanavunja sheria kwa kusababisha uvunjifu wa amani nchini na hivyo mkono wa sheria utawafikia.”
 
TRA imebaini kuwa baadhi ya watu wanaoshurutishwa kufunga biashara sio walengwa bali hutumika kuhalalisha azma ya wale wenye nia mbaya TRA imekuwa ikipokea taarifa na maombi kutoka kwa baadhi ya wafanyabishara na wananchi wema wakiomba ulinzi ili wafungue maduka yao na kufanya biashara maana ndio ajira yao na mahali pakujipatia riziki ya kila siku.
 
“Ifahamike kwamba wale wote wanaoshinikiza na kulazimisha wenzao kugoma wanavunja sheria kwa kuwalazimishwa wafanyabiashara kugomea agizo halali la kisheria hivyo kwa wale wote wanaotishiwa au kushurutiswa watoe taarifa kwa kupiga simu namba zifuatazo 0786 800 000, 0713 800333, 0800 110016 au barua pepe info@tra.go.tz,” ilisema taarifa.