RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Rished Bade kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kulingana na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, uteulzi huu umaanza tarehe 06 Mei, 2014. Bade anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Harry Kitilya ambaye alistaafu tarehe 14 Desemba, 2013.
Kabla ya uteuzi huo, Bade alikuwa Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania tangu Septemba, 2012 na baadaye kukaimu nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania tangia Bwana Kitilya alipostaafu. Kabla ya kujiunga na Mamlaka ya Mapato Tanzania, Rished Bade amewahi kufanya kazi katika maeneo mbalimbali yaliyompa ujuzi na weledi mkubwa kwenye mambo ya fedha na mapato.
Bade amewahi kufanya kazi kama Mkaguzi wa Benki za Biashara, Benki Kuu ya Tanzania, Oktoba, 1995 – Mei, 2000, Credit Manager, Akiba Commercial Bank, Juni, 2000 – Juni, 2001, Chief Financial Officer, Akiba Banking Corporation, Juni, 2001 – Septemba, 2001 na kama Chief Operating Oficer, Barclays Bank (Uganda), Septemba, 2001 – Machi, 2006.
Nafasi nyingine ni pamoja na Chief Executive Officer, Barclays Bank (Tanzania), 2007 – 2009, Chief Financial Officer, (East and West Africa Cluster) Barclays Bank Plc Emerging Markets, 2009 – 2012, na Chief Executive Officer, Tanzania Mortgage Refinance Company 2010 – 2012.
Rished Bade ana Shahada ya Kwanza ya Bachelor of Commerce and Management ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1995); Shahada ya Master of Commerce in Banking and Finance ya Chuo Kikuu cha Sydney (1999), na ni Certified Public Accountant (CPA).
Katika kumteua kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Rais ana imani kubwa kwa elimu, uzoefu na weledi alionao, Rished Bade kwa kushirikiana na watumishi wenzake, atatoa mchango mkubwa kwa Taifa kwa kuzidi kuimarisha Mamlaka hiyo na kuboresha utendaji wake na hivyo kuongeza mapato ya Serikali kwa faida ya Taifa.