WAKATI Maonesho ya 35 ya Biashara ya Kimataifa ya Saba Saba yakitangazwa kuanza jana jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere bado idadi kubwa ya mabanda ya maonesho katika viwanja hivyo hayajafunguliwa na wahusika wameonekana wakiendelea na maandalizi kukamilisha hatua mbalimbali katika mabanda yao.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao huu jana katika viwanja hivyo ulibaini idadi kubwa ya mabanda ya maonesho bado hayajafunguliwa na wafanyabiashara wengine walikuwa wakiendelea na kumalizia ujenzi wa mabanda yao.
Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata zilieleza kuwa kwa wafanyabiashara wa nje wamekwamishwa na Mamla ya Mapato nchini (TRA) ambao wamechelewesha baadhi ya mizigo (makontena) ya wafanyabiashara hao ambayo mengine yametolewa usiku wa kuamkia jana.
“Unajua kwa sisi kutoka nje tumecheleweshwa na taratibu za TRA kwani wengine tumepewa mizigo yetu jana usiku, na hivi tunavyozungumza wengine hadi sasa bado wanaendelea na hatua mbalimbali ya kutoa makontena yao bandarini,” alisema mmoja wa wafanyabiashara kutoka nje ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini kwani si msemaji.
Aliongeza kuwa kwa upande wao baadhi wamekwamishwa na mfumo wa utoaji mizigo ambao umekuwa ukitumia muda mrefu kiasi cha kupoteza muda kwa mteja kabla ya kupatiwa mzigo wake hasa kutoka nje ya nchi.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), maonesho ya mwaka huu yameanza tangu jana (Juni 28, 2011) na yatafanyika kwa siku 11, ambapo yatafungwa Julai 8, 2011.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mabanda yote yatakuwa yakifunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa kwa pamoja saa tatu usiku, huku kila mmiliki akitakiwa kukatia bima bidhaa zake ili kujikinga na hatari/hasara anuai zinazoweza kujitokeza ndani ya maonesho hayo.
Aidha taarifa imebainisha kuwa upigaji wa muziki kwa sauti ya juu kiasi cha kuleta usumbufu kwa wengine wakati wa maonesho hauta ruhusiwa, huku TANTRADE ikipiga marufuku uuzaji wa bidhaa zote za madawa pasipo idhini ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).
Juhudi za kumpata Mkurugenzi wa TANTRADE, Ramadhan Khalifan kutoa ufafanuzi juu ya suala hilo hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuita muda wote bila kupokelewa.