TRA Yakusanya Milioni 84.6 Mwezi Agosti

Na Ally Daud-MAELEZO

MAMLAKA ya mapato nchini (TRA) imefanikiwa kukusanya asilimia 92 sawa na shilingi milioni 84.618 kwa mwezi Agosti mwaka huu ikiwa ni katika kutimiza lengo la kukusanya bilioni 1 na kuendelea kila mwezi kwa Mkoa wa kodi Ilala.
Hayo yamesemwa na Afisa Elimu na Huduma wa TRA Mkoa wa kodi Ilala Bw. Zakeo Kowero katika semina iliyofanyika jijini Dar es salaam kati ya mamlaka hiyo na watendaji wa kata na Serikali za Mitaa wilaya ya Ilala kuhusu maswala ya ukusanyaji kodi bora na sahihi kwa maendeleo ya Wilaya na nchi kwa ujumla.

Bw. Kowero amesema kuwa kiasi hiko kimekusanywa kwa mwezi agosti kufuatia malengo waliojiwekea kama Wilaya na kuhakikisha wanapiga hatua zaidi ya hapo ili kuhakikisha mapato yanapatikana kwa wingi kwa maendeleo ya nchi.
“tumejiwekea maelengo ya kukusanya mapato kuanzia shilingi bilioni moja na kuendelea kwa mwezi lakini tumefanikiwa kukusanya milioni 84 ikiwa ni katika kutimiza malengo yetu na tunaimani ya kufanya vizuri kwa watendaji wetu wamejipanga kwa utendaji na uadilifu katika ukusanyaji mapato” alisema Bw. Kowero.

Mbali na hayo Bw. Kowero amesema kuwa semina hiyo ya kukutana na watendaji hao inalenga kutatua kwa wakati kero za na matatizo ya walipaji kodi ikiwa pamoja na kutumia mashine za EFD kwa usahihi katika ukusanyaji kodi wao. Aidha Bw. Kowero ameongeza kuwa katika semina hiyo inawaelimisha watendaji hao kuweza kuimarisha uhusiano mzuri kati ya TRA na walipa kodi ili kuhakikisha wanafatilia kwa urahisi madeni ya wasiolipa kodi kwa wakati muafaka.

Afisa huyo wa Elimu na huduma TRA Mkoa wa kodi Ilala amewataka wanaokwepa na wasiolipa kodi wajisalimishe wenyewe ili kuweza kulipa madeni wanayodaiwa kabla mkono wa sheria haujaanza kuwatafuta.