TRA Kugawa Bure Mashine za EFD kwa Wafanyabiashara Wadogo Dar

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alfayo Kidata

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alfayo Kidata

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza utaratibu wa kuanza kuwagawia bure Wafanyabiashara wadogo na wakati Mashine za EFD kwa awamu. Akitoa taarifa hiyo kwa umma Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alfayo Kidata alisema utaratibu wa kutoa mashine hizo kwa Wafanyabiashara wa Kati na Wadogo litafanyika kwa utaratibu waliouweka.

Alisema katika awamu ya kwanza TRA itaanza kugawa Mashine za EFD kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es salaam wapatao 5,703. Alisema Wafanyabiashara hao 5,703 watakaopata mashine hizo ni wale wenye mauzo ghafi kati ya “shilingi milioni 14 na milioni ishirini (20) kwa mwaka.

Aidha alisema wafanyabiashara waliopo kundi hilo wafike katika ofisi za Mamlaka ya Mapato za Mikoa wanayolipia kodi ya Ilala, Kinondoni na Temeke ilikuhakiki usajili wao, huku wakiwa na namba ya utambulisho wa Mlipakodi (TIN), na kupata kibali cha kupewa Mashine ya EFD kuanzia tarehe 01 Juni, 2016.

“…Wafanyabiashara watatakiwa kwenda na nakala ya cheti cha TIN, Picha mbili ndogo(Passport size, leseni ya biashara, namba ya simu ya kiganjani, na maelezo kamili ya sehemu wanayofanyia biashara, kama jina la mtaa, namba nyumba na au jina la eneo maarufu liliopokaribu na wanapofanyia biashara,” alisema Kidata.

Alisema baada ya kupata kibali Mfanyabiashara atakwenda kuchukua Mashine ya EFD kutoka kwa mmojawapo wa Wasambazaji wa EFD walioidhinishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ambao ni kampuni za Pergamon Group Ltd, Bolsto Solutions Ltd, Advatech Office Supplies Ltd, Compulynx Tanzania Limited, Web Technologies Ltd, Softnet Technologies Limited, Maxcom Africa Limited na Power Computers and Telecommunication Limited.

Akifafanua zaidi juu ya zoezi hilo alisema mfanyabiashara ataingia mkataba wa huduma baada ya mauzo na Msambazaji kwa ajili ya kupewa huduma ya matunzo na matengenezo ya Mashine ya EFD.

“Wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es salaam watakaobaki na wale wa Mikoa mingine wanaostahili kupewa Mashine za EFD bila malipo watapewa Mashine hizo katika awamu ya pili. Tunapenda kusisitiza kwamba, Wafanyabiashara wote wanaotakiwa kutumia Mashine za EFD kutunza kumbukumbu za biashara na kutoa risiti, watumie Mashine hizo kikamilifu na ipasavyo kwa hiari bila kushurutishwa,” alisema.