TRA kuanza kurudisha VAT kwa wageni

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya

Na Joachim Mushi

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) itaanza kurejesha kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa raia wa kigeni watakapokuwa wakiondoka nchi ili kuongeza ushawishi wa raia hao kununua bidhaa nchini.

TRA itaanza kufanya marejesho hayo ya kodi kwa wageni Januari Mosi 2012, hatua ambayo inatajwa kuwa itaongeza manunu ya bidhaa mbalimbali za nchini kwa raia kutoka nchi za nje.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Saleh Mshoro amesema mabadiliko hayo yanaanza baada ya bunge la bajeti lililopita kupitisha sheria ambayo inaruhusu TRA kufanya marejesho ya VAT.

Mshoro amesema kitendo cha kurudishiwa ongezeko la thamani kwa fedha ambayo wageni hao waliitumia wakati wakinunua bidhaa anuai nchini, itasaidia wengi kununua bidhaa zetu- kwani mbinu hiyo imekuwa ikitumiwa pia na nchi za Kusini mwa Afrika.

Mshoro amesema ili mgeni aweze kurejeshewa makato hayo anapokuwa akitoka nje itamlazimu kuwa na hati ya kusafiria, tiketi ya kuruhusiwa kupanda ndege pamoja na bidhaa husika ambazo zitahakikiwa na maofisa wa TRA na mawakala.

Ameongeza kuwa tayari TRA imewajulisha mabalozi wa Tanzania wan chi mbalimbali kuhamasisha wananchi kutoka nchi hizo kuja kufanya manunuzi kwa bidhaa Tanzania kwani watapata punguzo.

Aidha amevitaja vigezo vitakavyotumika kutoa msamaha huo kuwa ni pamoja na bidhaa hiyo kuwa haijafunguliwa tangu iliponunuliwa, iwe imenunuliwa si zaidi ya miezi sita na yenye thamani zaidi ya kuanzia laki nne na zaidi.