Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi juu ya uwezekano wa kunyesha mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya nchi ambayo huwenda ikaleta madhara. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam na Ofisa Uhusiano wa TMA, Monica Mutoni maeneo ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua hizo ni pamoja na mikoa ya Singida na Dodoma, Iringa, Mbeya na Njombe na Mikoa ya Ruvuma na Morogoro.
Alisema kwa mujibu wa vipimo, mvua hizo za zaidi ya mm 50 ndani ya saa 24 zinatarajia kunyesha kuanzia Februari 19 hadi 21, 2014 hivyo TMA imewataka wananchi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari juu ya madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na mvua hizo kwa maeneo tajwa.
Taarifa imefafanua kuwa hali hiyo imesababishwa na kuimarika kwa mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika rasi ya Msumbiji, kitendo kitakachosababisha kuvuta upepo kutoka misitu ya Congo kupitia maeneo tajwa hivyo kukubwa na mvua hizo.
“…Idara zinazohusika na hali ya tahadhari pamoja na wakazi wa maeneo hatarishi wanashauriwa kuchukua tahadhari. Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo kila itakapobidi,” ilisema taarifa hiyo ya TMA.