MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi wanaotoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, pomoja na mikoa ya Arusha, Manyara kutokana na vipimo vya utabiri kuonesha uwezekano wa kunyesha mvua kubwa inayoweza kuleta madhara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo leo jijini Dar es Salaam, Vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimita 50 ndani ya saa 24 kila siku vinatarajiwa kunyesha kwa kiwango cha uhakika cha wastani wa asilimia 60 kwenye maeneo tajwa.
Taarifa hiyo imeyataja maeneo mengine ambayo yanayotarajiwa kuathirika kuwa ni pamoja na mkoa wa
Kilimanjaro, Mkoa wa Mara, Mkoa wa Mwanza, Mkoa wa Simiyu, Geita na pamoja na Kagera. Taarifa hiyo imefafanuwa kuwa mvua hiyo inatarajiwa kuanza kunyesha leo, Machi 13 hadi 15, 2014.
“…Hali hii inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua katika maeneo yaliyotajwa hapo juu. Tunatoa angalizo kuwa wakazi wa maeneo hatarishi, watumiaji wa Bahari pamoja na mamlaka zinazohusika na maafa, wanashauriwa kuchukua tahadhari stahiki,” imeeleza taarifa hiyo ya TMA.
Hata hivyo taarifa hiyo imesema mvua zinazoendelea na zinazotarajiwa kunyesha ni muendelezo wa mvua za msimu wa masika katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hii na itatoa mrejeo kila itakapobidi.