MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewatahadharisha wakazi wa maeneo yote ya ukanda wa Pwani nchi kuchukua tahadhari kwani vipimo vya hali ya hewa vimeonesha huenda ukavuma Upepo mkali pamoja na mawimbi makubwa katika maeneo yote ya ukanda wa pwani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo, imebainisha kuwa upepo huo utakuwa mkali kufikia kilomita 40 kwa saa pamoja na mawimbi makubwa kuzidi mita 2.0 katika ukanda wote wa pwani hali ambayo huwenda ikaleta madhara kwa wakazi wa maeneo hayo
“….Hali hii inatokana na kuimarika kwa mfumo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika Bahari ya Hindi, karibu na visiwa vya Comoro. Mfumo huu unatarajiwa kuvuta upepo kutokea pwani ya Somalia. Kuna uhakika wa asilimia 60 kutokea kwa hali hiyo,” ilisema taarifa ya TMA.
Aidha taarifa hiyo imeyataja maeneo ambayo huenda yakaathiriwa na hali hiyo kuwa ni pamoja na Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba; hivyo wakazi wa maeneo hayo kuombwa kuchukua tahadhari. Hata hivyo Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia hali hiyo na itatoa mrejeo zaidi.