Tishio la Maandamano ya Waislamu; Ukimya Watawala Dar, Shughuli Zasimama, JWTZ Waingia Mitaani

Baadhi ya magari ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) wakionekana kudhibiti ulinzi maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. (Picha na Michuzi Blog)

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

HALI ya ukimya leo imetawala katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hasa kati kati ya jiji na hata maeneo ambayo kikawaida huwa na misongamano mikubwa ya watu. Maeneo ya Kariakoo ambayo huwa na idadi kubwa ya watu hata kwa siku za Siku Kuu leo haikuwa hivyo, kwani yalionekana matupu na makundi ya askari wakionekana kuweka kambi ama kuzunguka hapa na pale kuimarisha ulinzi.

Hali hii imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za baadhi ya Waislamu kutaka kuandamana kuelekea Ikulu mara baada ya swala ya Ijumaa wakipinga kitendo cha kukamatwa kwa mmoja wa viongozi wa taasisi za Uislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na kushikiliwa kwa baadhi ya Waislamu ambao walikamatwa katika vurugu za uvamizi wa makanisha hivi karibuni eneo la Mbagala Jijini Dar es Salaam.

Shughuli za kibiashara hasa za maduka na nyinginezo ambazo huendeshwa pembezoni mwa Barabara ya Uhuru, Mitaa ya Kongo, Msimbazi, Mnazi Mmoja, Lumbumba na maeneo mengine ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam leo zilisimama na maduka kuonekana yamefungwa kutokana na kuhofia vurugu za waandamanaji.

Ulinzi wa Askari Polisi wa Kawaida, Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) ulikuwa mkali maeneo yote ya jiji, na baadhi ya maeneo mengine yalionekana magari ya wanajeshi waliokuwa wamevalia mavazi ya kutuliza ghasia wakionekana tayari kuongeza nguvu kwa Jeshi la Polisi.

Kama hiyo haitoshi polisi walitumia helkopta kufanya doria kuangalia usalama maeneo mbalimbali ya jiji. Helkopta ya Polisi ilisikika ikipita angani kwa kuzunguka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kuangalia hali yoyote ya machafuko. Hali ya wasi wasi pia ilionekana kwa baadhi ya watu na kujiami muda wote, kuhofia kujikuta wakiingia katika vurugu hizo.

Kwa mujibu ya kipeperushi ambacho mtandao huu umekipata kikionekana kuwa kimeandaliwa na baadhi ya washawishi wa maandamano ya leo kinasema; Waislamu wanapaswa kuandamana wakipinga kitendo cha kushikiliwa kwa Sheikh Ponda, kutoweka kwa Sheikh Farid Mjini Zanzibar juzi na kitendo cha kushikiliwa na kufunguliwa kesi Waislamu waliokamatwa katika vurugu zilizotokea hivi karibuni maeneo ya Mbagala na kuchomwa moto kwa baadhi ya makanisa.

Hata hivyo licha ya Jeshi la Polisi kuweka ulinzi huo maeneo mbalimbali jioni baadhi ya Waislamu waliokuwa wakitoka kuswali walipambana na askari polisi pale walipojaribu kuandamana wakidai wanakwenda Ikulu. Askari walidhibiti maandamano maeneo ya Kariakoo na kuwakamata watu waliojaribu kupambana na askari waliokuwa wakilinda usalama.

Eneo la Ikulu Jijini Dar es Salaam na makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani napo ulinzi ulihimarishwa ili kuzuia vurugu zozote ambazo zingeweza kuibuka. Baadhi ya waandamanaji mmoja mmoja walijikuta wakikamatwa na polisi pale walipopenyeza na kujaribu kuibukia Ikulu huku wakiwa wameficha kanzu zao. Tunaendelea kufuatilia kwa karibu juu ya hali hiyo na kuwafahamisha wasomaji wetu.