Timu ya Simba Kupepetana na Kagera Sugar

Baadhi ya wachezaji wa Simba SC wakishangilia baada ya kufunga goli katika moja ya mechi zake

*Mbaga Kuchezesha Kenya, Uchaguzi TAFCA Wasogezwa

Na Mwandishi Wetu

LIGI Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi nane Oktoba 17 mwaka huu kwa mechi tano huku vinara wa ligi hiyo Simba wakiialika Kagera Sugar kutoka mkoani Kagera kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo namba 52 itachezeshwa na mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha wakati waamuzi wasaidizi ni Julius Kasitu na Methusela Musebula, wote kutoka Shinyanga. Mwamuzi wa akiba ni Ephrony Ndisa wa Dar es Salaam huku mtathimini wa waamuzi akiwa Charles Mchau kutoka Moshi.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale na Azam iliyo chini ya kocha Boris Bunjak kutoka Serbia. Nayo Polisi Morogoro iliyopanda msimu huu itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Mgambo Shooting ambayo imepata ushindi mara mbili mfululizo itakuwa nyumbani Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga ikiikaribisha Toto Africans katika mechi itakayochezeshwa na Geofrey Tumaini wa Dar es Salaam. Oljoro JKT inayonolewa na Mbwana Makata itakuwa nyumbani Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha dhidi ya African Lyon.

Wakati huo huo; Mwamuzi Oden Mbaga wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ndiye anayechezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana).

Mechi hiyo inachezwa leo Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi. Mbaga anasaidiwa na waamuzi wasaidizi wa FIFA, John Kanyenye kutoka Mbeya na Erasmo Jesse wa Morogoro.

TFF imeteua waamuzi hao baada ya kupata maombi kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ambao ndiyo waandaaji wa mechi hiyo ambayo ni moja ya vipimo kwa kocha mpya wa Harambee Stars, Henry Michel kutoka Ufaransa.

Wakati huo huo; Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama hicho ambao sasa utafanyika Novemba 25 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.

Hivyo, amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.