Timu ya Azam Fc Wamsajili Mbaya wa Yanga Sc

azam

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, umefanikiwa kunasa saini ya mshambuliaji nyota wa timu ya Medeama ya Ghana, Enock Atta Agyei, ambaye tayari amesaini mkataba wa miaka miwili.

Kinda huyo anatua baada ya kulivutia Benchi la Ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Zeben Hernandez, ambaye amependekeza asajiliwe baada ya kumuona kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Medeama ikiilazimisha sare ya bao 1-1 Yanga katika mchezo wa Kundi A wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Uongozi wa mabingwa hao umefanya jitihada za hali ya juu hadi kunasa saini yake, ambapo umelazimika kumpandia ndege mshambuliaji huyo hadi mjini Takoradi, Ghana, usajili huo ukiratibiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba, aliyeenda huko na kukamilisha vema kazi hiyo maalumu kwa kuzungumza na pande zote mbili mchezaji na mmiliki wa Medeama, Moses Armah.

Akiwa nchini Ghana, Kawemba alipata fursa ya kukutana na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Ghana ‘Black Stars’, Avram Grant raia wa Israel, wakati wa mchezo wa marudiano kati ya Medeama na Yanga ulioisha kwa wenyeji kushinda mabao 3-1.

Katika mazungumzo yake na Kawemba, Grant aliyewahi kuifundisha Chelsea na kuifikisha kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008, aliipongeza Azam FC kwa kutambua kipaji cha Enock na kumsajili.

Enock, 18, mwenye kipaji cha hali ya juu, mara baada ya kukamilisha taratibu zote za kujiunga na Azam FC, anatarajia kutua nchini kesho Jumamosi saa 2.15 asubuhi na ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ).

Straika huyo mwenye kipaji cha hali ya juu anayetabiriwa kutikisa miaka ijayo, ameanza kung’ara wakati akiwa hana uzoefu mkubwa wa Ligi Kuu ya Ghana kwani amejiunga na Medeama Desemba mwaka jana baada ya kufanya vizuri akiwa na Windy Professionals ya Ligi Daraja la Kwanza nchini humo.

Chanzo: azamfco.tz