Na Mwandishi Wetu
TIKETI kwa ajili ya mechi namba 78 kati ya Yanga na Simba itakayochezwa Oktoba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitaanza kuuzwa kesho saa 4 asubuhi katika vituo vitano tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Boniface Wambura amesema vituo vitakavyouza tiketi hizo vitaziuza hadi hadi saa 10 jioni.
Amevitaja vituo vitakavyouza tiketi hizo kuwa ni pamoja na Uwanja wa Taifa, kituo cha mafuta cha Oilcom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, kituo cha mafuta cha Big Bon kilichoko Msimbazi- Kariakoo na mgahawa wa Steers ulioko Mtaa wa Samora/Ohio.
Wambura ameongeza kuwa tiketi zitauzwa siku ya mchezo katika magari maalumu yatakayoegeshwa katika maeneo ya uwanja. Tunatoa mwito kwa mashabiki kununua tiketi zao mapema ili kuepuka bughudha ya kuingia uwanjani siku ya mechi.
“Viingilio katika pambano hilo ni sh. 5,000 kwa viti vya kijani na bluu (tiketi 36,000), sh. 7,000 viti vya rangi ya chungwa (tiketi 11,000) sh. 10,000 VIP C (tiketi 4,000), sh. 15,000 VIP B (tiketi 4,000) na sh. 20,000 VIP A (tiketi 700),” alisema Wambura.
Aidha amewataja waamuzi wa mechi hiyo kuwa ni Oden Mbaga (centre referee), Hamis Chang’walu (assistant 1) na John Kanyenye (assistant 2). Mtathimini wa waamuzi (referee assessor) ni Soud Abdi wakati kamishna wa mchezo huo ni Mohamed Nyange.