Tigo wamzawadia pikipiki ya mizigo mshindi mwingine


Ofisa Uhusiano wa Tigo, Jackson Mmbando (kushoto) akizungumza na mshindi wa pili wa droo ya pikipiki ya magurudumu matatu kwa njia ya simu alipokuwa akichezesha droo hiyo, kulia ni Mratibu wa Matukio kutoka Tanzania Solid Limited, Catherine Kasimbagi.

Na Joachim Mushi

KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Tigo imetoa zawadi ya pili kwa mshindi wa pikipiki ya miguu mitatu aina ya Toyo baada ya kuchezesha droo nyingine kwa washiriki wateja wa mtandao huo wanaocheza kwenye shindano hilo.

Mshindi huyo, Lewis Richard mfanyabiashara mkazi wa Tabata Chang’ombe alipatikana jana baada ya Tigo kuchezesha droo ya pili iliyosimamiwa na Ofisa Msimamizi wa Michezo ya Kubahati nchini (GBT), Abdallah Hemed ndani ya banda la kampuni hiyo kwenye Maonesho ya 35 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kupatikana kwa mshindi huyo, Ofisa Uhusiano wa Tigo, Jackson Mmbando alisema wameamua kutoa zawadi hizo kwani ni moja ya kifaa kinachoweza kumsaidia Mtanzania kufanya shughuli zake na hata kumuongezea kipato.

Alisema kwa sasa zimebaki pikipiki mbili aina hiyo ambazo nazo zitatolewa kwa washiriki wa mchezo huo baada ya droo mbili kuchezeshwa, moja ikitarajiwa kuchezeshwa Agosti Mosi na nyingine Septemba mwaka huu.

“Huyu ni mshindi wa pili (Richard) kwani Juni 20 tulimpata mshindi mwingine anayefahamika kama Yusuf Versi mkazi wa Songea (51), tunaomba wananchi waendelee kushiriki katika mchezo huu ili wajishindie zawadi hizi,” alisema Mmbando.

Mshiriki katika mchezo huo anatakiwa kutuma maneno yafuatayo; imani, akiba, thawabu, pesa, dunia, kondoo, shinda, nge, ng’ombe, kaa, mizani, ndoo, mshale, mbuzi, mashuke, mapacha, samaki, suna, amani, kisura, au neno Simba kwenda namba 15510 kwa sh. 158.4.