KAMPUNI ya Azam Media Limited, leo imetangaza kuwa Tido Mhando ameteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Uhai Production Ltd.(UPL). Tido, anaungana na Rhys Torrington ambaye ni Mkuregenzi Mtendaji Mkuu wa Azam Media Ltd na mtangazaji huyo maarufu wa mpira zamani nchini, Mhando ataanza majukumu yake mara moja, ikiwa jukumu lake kubwa ni utengenezaji na uboreshaji wa vipindi vya kitanzania katika televisheni na redioni.
Mhando mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 40 kwenye tasnia ya utangazaji na Uandishi wa Habari, ni mtu anayejulikana na kuheshimika katika tasnia hiyo ukanda wa Afrika Mashariki na Ulimwenguni kote. Tido Mhando sasa wa Azam TV Alianza kazi kama DJ Radio Tanzania na mnamo mwaka 1985 alijiunga na BBC idha ya Kiswahili Nairobi kama mwandishi wa habari. Ukuwaji wake ndani ya shirika ulimpelekea kuhamishiwa jijini London mwaka 1991 ambapo aliteuliwa kuwa Mwafrika wa kwanza kuongoza idara ya Idhaa ya Kiswahili BBC.
Baada ya kurejea Tanzania, Mhando ameshika nyadhifa mbali mbali za juu zikiwemo Mkurugenzi Mkuu wa TBC na hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Mwananchi Communication Ltd. Akizungumzia uteuzi wake, Mhando amesema; “Ninayo furaha kubwa kujiunga na Azam Media, pia na changamoto kubwa zilizopo mbele yetu kuifanya kuwa kampuni pekee ya Televisioni na Redio yenye ubora katika kutoa burudani hapa nchini (Tanzania) pia na ukanda wote wa Afrika,”.
Mhando ofisi zake zitakuwepo katika jengo la kisasa la Uhai Production Tabata, Dar es Salaam. UPL inajulikana kwa ubora wake katika kurusha matangazo yake moja kwa moja kama vile, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na vipindi vingine maarufu kama Kwetu House na Morning Trumpet. Pia katika wiki zijazo UPL itazindua studio zake mpya zenye kiwango cha kimataifa ambazo itamuwezesha Mhando kuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza vipindi mbali mbali vyenye viwango vya kimataifa akishirikiana na watengenezaji wazawa.
Akizungumzia uteuzi huo, Muingereza Torrington amesema: “Tunayo faraja kubwa kwa Tido kujiunga nasi wakati tunakaribia kutimiza mwaka wetu wa kwanza tokea tuanze kutoa huduma, inanipa furaha kwamba Azam TV imekuwa kwa kasi na kuwa wasambazaji wakuu na watoa huduma bora satellite Pay Tv Tanzania,”.
“Kwa uzoefu wake nategemea Tido atachukuwa jukumu la kutupeleka katika hatua nyingine ya mafanikio kibiashara kwa kutengeneza vipindi na burudani mbalimbali kwajili ya wateja wetu Tanzania na kuvuka mipaka yetu. Na mtakia kilala kheri katika majukumu yake mapya,” amesema.