Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwasili nchini Japan Mei 29, 2013, kushiriki katika Mkutano wa Tano wa Kuzungumzia Maendeleo ya Afrika ujulikanao kama Tokyo International Conference on African Development (TICAD – V) uliopangwa kufanyika mjini Yokohama Juni Mosi hadi 3, mwaka huu, 2013.
Rais Kikwete amealikwa kushiriki katika Mkutano huo na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, mkutano huo pia utaadhimisha miaka 20 tokea kuanzishwa kwa mchakato wa mikutano ya TICAD.
TICAD V utawashirikisha viongozi wa Afrika, viongozi wa Japan na washirika wa maendeleo ya Afrika ikiwamo Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na utafunguliwa na Waziri Mkuu wa Japan, Mheshimiwa Abe.
Wengine waliopangwa kuzungumza kwenye sherehe hiyo ya ufunguzi wa Mkutano huo mkubwa ni Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Hailemariam Desalegn ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika Dkt. Nkosazana Dlamini Zuma.
Katika tukio lake la kwanza kubwa baada ya kuwasili nchini Japan, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Abe katika mkutano uliopangwa kufanyika mjini Tokyo. Mbali na kukutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu, Rais Kikwete pia atakuwa miongoni mwa kundi la viongozi wa Afrika watakaokutana na Mfalme wa Japan, H.M. Akihito.
Katika mkutano kati ya viongozi hao wawili, Waziri Mkuu wa Japan anatarajiwa kuwa atatangaza kuwa Japan inaifutia Tanzania deni la dola za Marekani milioni 220 likiwa ni deni la mchele ambao Tanzania iliupata kutoka Japan chini ya mikataba iliyotiwa saini kati ya mwaka 1980 na 1983 kati ya Mamlaka ya Chakula ya Japan na Serikali ya Tanzania.
Aidha, inatarajiwa kuwa Abe atatangaza rasmi kuwa Japan itagharimia ujenzi wa barabara ya juu kwa juu (fly-over) katika eneo la Ubungo, Dar es Salaam, kama moja ya hatua za kupunguza msongamano katika jiji hilo.
Mbali na kuungana na viongozi wenzake wa Afrika kuhudhuria mkutano wa TICAD V, Rais Kikwete pia anatarajiwa kukutana na kuzungumza na wakuu wa mashirika makubwa na kimataifa ya kibiashara na uchumi ya Japan ambayo yanapenda ama kuimarisha shughuli zake za uzalishaji ama kuanzisha shughuli mpya katika Tanzania.
Miongoni mwa viongozi wa mashirika ambayo Rais Kikwete atakutana nayo ni wa Somitomo Corporation ambayo inashiriki katika kuendeleza miradi ya umeme katika Tanzania, Nitori Holding ambalo linajaribu kuwekeza katika sekta ya nguo na kilimo cha pamba katika Tanzania na Mitsubishi Corporation ambalo liko katika shughuli za utafutaji gesi asilia na mafuta.
Mkutano wa TICAD V miongoni mwa mambo mengine utajadili mchango wa sekta binafsi, biashara na uwekezaji kama injini za maendeleo, jinsi gani Afrika inavyoweza kuimarisha sekta ambazo zimejithibitisha kuwa misingi ya kukua kwa uchumi wa Bara la Afrika, Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015 ambao ni mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDG’s). Hatimaye, mkutano huo utatoa Azimio ya Yokohama 2013 na Mpango wa Utekelezaji wa Yokohama kwa miaka 2013 hadi 2017.
Mikutano ya TICAD (TICAD Policy Forum and Conference) ilianzishwa mwaka 1993 na Japan kwa kushirikiana na UN, UNDP na Benki ya Dunia kwa njia ya kujadili na kuendeleza ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika.
Chini ya mchakato huo wa TICAD, Japan hujenga mazingira ya kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Bara la Afrika ambalo nalo ndilo linamiliki na kuongoza jukumu ya kimsingi la kujiendeleza kwa kushirikiana na Bara la Asia na Jumuia ya Kimataifa.
Tokea ulipofanyika mkutano wa kwanza – TICAD 1 mjini Tokyo Oktoba 5-6, mwaka 1993, imefanyika mikutano mingine mitatu na kujenga mazingira mazuri zaidi ya jinsi Japan na Jumuia ya Kimataifa inavyoweza kuchangia maendeleo ya Afrika.