Thomas Mashali ‘Awatusi’ Mabondia Wenzake

Bondia Thomas Mashali akionesha midoli yake anayoifananisha na mabondia wenzake, Kalama Nyilawila (kushoto) na Mada Maugo, wakati wa mazoezi yake yanayoendelea katika gym yake iliyopo Manzese, Dar es Salaam (Picha na BLOG YA SUPER D)


BONDIA Thomas Mashali amewatusi mabondia wenzake Mada Maugo na Kalama Nyilawila kwa kuwafananisha na midoli na kuwakebehi kuwa si chochote wala lolote kwake.

Hatua hiyo ya Mashali inatokana na awali kupondwa na Maugo kuwa hana uwezo na ni heri akageukia biashara ya kuuza chapati, wakati Kalama akimkebehi kuwa ni kibonde wake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika chumba chake maalumu kwa mazoezi (gym) eneo la Manzese, Dar es Salaam, Mashali alisema mabondia hao hawana uwezo wa kupambana na yeye kwa sasa na anawafananisha na midoli kwake.

Mashali, ambaye atapanda ulingoni Oktoba 30 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee kuzichapa na Maugo, yuko katika mazoezi makali kwa ajili ya pambano hilo kabla ya baadaye kupigana na Nyilawila.

“Unajua hawa ni kama midoli kwangu (huku akionesha midoli aliyoshika), na kwa kudhihirisha hilo nitaanza na maugo Oktoba 30 kumuonesha kuwa hatakiwi kuzungumza asichokijua,” alisema Mashali. Alisema anaamini uwezo wake wa sasa utakuwa wa juu zaidi ya Maugo na Nyilawila, ambapo alipata sare alipopigana na Nyilawila.

Katika pambano hilo la Mashali na Maugo la Oktoba 30, kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi, ambapo Ibrahim Class ‘King Class Mawe’ atapanda ulingoni kupambana na Halid Manje katika mchezo wa raundi sita.