TheHabari Yaomboleza Kifo cha Zig Ziglar

Hayati Zig Ziglar enzi za uhai wake

MTANDAO huu unaungana na wamarekani pamoja na wadau wengine duniani walioutambua na kuuthamini mchango wa gwiji la uhamasishaji hapa Marekani na duniani kwa ujumla, Mzee Zig Ziglar. Mzee huyu alikuwa ni hodari sana katika fani ya Uhamasishaji (The Art of Motivational Speaking) na aliweza kuwasaidia watu wengi kubadili muelekeo wa maisha yao katika nyanja za kielimu, kibiashara,kijamii, na kimaisha kwa ujumla kupitia semina, vitabu, na CD, ambazo zinapatikana maeneo mengi duniani (Ikiwemo Tanzania).

Mzee Ziglar atakumbukwa kwa vitabu vyake vya uhamasishaji kama “See you at the Top”(1975), “Raising Positive Kids in a Negative World”(1985), “Over the Top”(1994), na vingine vingi, ambavyo viliandikwa katika umahili wa hali ya juu. Mzee Ziglar pia anaheshimika kwa misemo ya busara kama “Where you start is not as important as where you finish”, akiwa na maana kwamba “Ulipoanzia sio muhimu sana kama utakapo malizia” na “If you can dream it, then you can achieve it” yaani “Kama ukiweza kukiota, basi unaweza ukakipata”. Hayo ni baadhi tu ya maneno ambayo ametuachia mzee wetu huyu na kwahakika watu wengi wameshanufaika, na wengi tunaendelea kunufaika kupitia busara zake hizo.

Mzee Ziglar alizaliwa Coffee County, Alabama(USA) na amefariki jana kule Plano, Texas(USA) baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa mapafu (Pneumonia) kwa muda mrefu. Mpaka anafikwa na umauti, Ziglar alikuwa na umri wa miaka 86 na ameacha mke, watoto, na wajukuu kadhaa. Misa ya kumuombea Mzee Ziglar itafanyika siku ya Jumamosi, tarehe 1/12/2012 katika kanisa la Prestonwood Baptist huko huko Plano, Texas (USA).

Mungu ilaze roho ya marehemu Ziglar mahala pema peponi, Amen

Imetayarishwa na Rungwe Jr.
TheHabari.com