TGNP Mtandao wamekutana na Kamati za Bunge Mjini Dodoma katika warsha ya siku moja iliyofanyika katika ukumbi wa Hazina ndogo. Warsha hiyo ililenga kuwawezesha Wabunge zaidi ya 100 kushiriki katika kuhakikisha bajeti inayoandaliwa na Serikali inakuwa katika mrengo wa kijinsia.
Semina hiyo pia imelenga kuwawezesha wabunge kutambua masuala yanayowakabili wanawake na makundi yaliyoko pembezoni na kudai yaingizwe kwenye bajeti ikiwemo kutengewa fedha. Aidha ni kuwaongezea watunga sera hao uelewa kuhusu Tamko la bajeti ya kijinsia (Gender Budget Statement) na matumizi yake kama nyenzo ya kufanikisha malengo ya bajeti yenye mtazamo wa kijinsia.
Warsha hiyo iliendeshwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi na wanachama wa TGNP Aseny Muro na Gemma Akilimali ambao walitoa mada na kujibu maswali mbalimbali kutoka kwa wabunge hao wakisaidiana na wafanyakazi wa TGNP na Chuo cha Mafunzo ya Jinsia (GTI).