UZINDUZI WA ILANI YA MADAI YA WANAWAKE KWENYE KATIBA MPYA
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni asasi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kupigania usawa wa jinsia, kukuza uwezo wa wanawake, kustawisha na kubadilisha mfumo wa kijamii ambao unambagua, unamnyonya na unamkandamiza mwanamke kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii.
TGNP kwa kushirikiana na wanaharakati wa masuala ya ukombozi wa wanawake, usawa wa Kijinsia, haki za Binadamu, Demokrasia, Utawala bora na Maendeleo tumekuwa na utaratibu wa kuandaa Ilani mbalimbali za wananchi kuanzia uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010. Mwaka huu tumeandaa “Ilani ya Madai ya wanawake wa Tanzania kwenye Katiba mpya” ili kuwezesha jamii kuchambua, kujadili na kuangalia maeneo muhimu ya kudai uwajibikaji na utekelezaji wakati wa mijadala ya kuandaa katiba mpya .
Mchakato wa kuandaa madai ya Katiba Mpya umetokana na ushiriki mkubwa wa wadau mbalimbali. Kwanza kabisa ni mashirika mbalimbali katika ngazi ya kitaifa na jamii yanayotetea haki za binadamu, jinsia na maendeleo, FemAct, wadau wa mikutano ya kila Jumatano (GDSS) inayofanyika katika viwanja vya TGNP Mabibo. Katika vipindi tofauti semina hizi zilitoa nafasi ya ushiriki wa makundi mbali mbali ya kijamii hususan walioko pembezoni, yakiwemo makundi ya wenye ulemavu, wanaoishi na VVU/UKIMWI, vijana, wazee, wajasiriamali, wakulima na wafugaji wadogo wadogo, ambapo wanawake, wanaume, Vijana na watoto wamepata fursa ya kujadili na kutoa mapendekezo yaliyoainishwa katika Ilani hiyo. Pia ushiriki wa makundi ya kijamii kupitia mchakato wa uraghbishi katika wilaya za Kishapu, Mbeya Vijijini na Morogoro; pamoja na Tamasha la Jinsia ngazi ya jamii lililofanyika wilaya ya Morogoro Vijijini.
Vile vile TGNP ilishiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Mfuko wa Wanawake Tanzania (WFT) lililohusisha wanawake takribani 110 kutoka taasisi zaidi ya hamsini zilizowakilisha asasi mbalimbali kutoka mikoa 19 ya Tanzania bara na visiwani tangu tarehe 22-24 Oktoba 2012. Kongamano hili lilijadili na kukubaliana masuala ya msingi ya madai ya wanawake katika katiba mpya.
Tunaamini kwamba madai haya yametokana na ushiriki na sauti mbalimbali za wadau wanaotetea haki za wanawake na hususani haki zao za kikatiba na tunaamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba inatambua changamoto zinazowakabili wanawake na vijana wa kike hasa walioko pembezoni na itayatafanyia kazi madai ya wanawake ili yaweze kuingizwa katika katiba mpya. Madai ya Wanawake wa Tanzania katika Katiba Mpya ni mwafaka wa kitaifa unatokana na mwendelezo wa harakati za raia na hususani za wanawake za kutaka mabadiliko ya msingi ya kimfumo, kisera na kisheria yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto zitokanazo na mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi wa dunia, mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano, na kuimarika kwa mifumo kandamizi inayoashiria kumbebesha raia maskini na hasa mwanamke mzigo mkubwa zaidi kutokana na changamoto za mabadiliko haya.
Kwa mfano msukosuko wa kiuchumi uliozikumba nchi za kibepari tangu mwaka 2008, umezifanya nchi hizi chini ya uongozi wa matajiri wachache wa dunia, kujizatiti zaidi katika kupora rasilimali za nchi zetu wakishirikiana na viongozi wachache na mabepari wa nchi zetu wakiwemo wanaume na hata wanawake.
Sisi Wanawake tunataka katiba inayotokana na mchakato uliyoshirikisha sauti za wanawake na wanaume, na itakayoweka bayana makubaliano ya misingi mikuu itakayoongoza nchi yetu. Vilevile tunataka katiba iliyojengewa misingi ya usawa, utu na inayokataza aina zozote za ubaguzi na unyanyasaji wa kijinsia.
Ilani ya madai ya wanawake wa Tanzania katika katiba mpya imeainisha madai 18 madai hayo ni pamoja na:
• Katiba iwe na mrengo wa Jinsia, hii pamoja na kutambua kuwa katiba ni mali ya watanzania wote wanawake na wanaume hivyo iwekwe kwenye lugha nyepesi itakayowawesha wanawake kuitumia katika kulinda, kutetea na kudai haki zao.
• Haki za wanawake zibainishwe kikamilifu katika katiba mpya kupitia katika tamko la msingi la haki za binadamu ( Bill of Rights)
• Katiba iweke misingi ya kulinda utu wa mwanamke ikiwa ni pamoja na maamuzi juu ya afya na miili yao
• Katiba mpya ibatilishe sheria zote kandamizi ikiwemo sheria ya ndoa, mirathi n.k
• Mikataba ya kimataifa na kikanda kuhusu haki za wanawake na watoto wa kike iwe sheria za nchi pale tu nchi inaporidhia ili kurahisisha utekelezaji
• Katiba iweke misingi ya itakayowezesha kuweko kwa mazingira ya upatikanaji wa haki sawa mbele ya sheria kwa wanawake na wanaume
• Katiba mpya ihakikishe afya ya uzazi inalindwa kikatiba.
• Katiba mpya iainishe haki za wanawake wenye ulemavu na wazee
• Katiba mpya iweke misingi ya kumwezesha mwanamke kushiriki katika uongozi katika nyanja mbali mbali kwa kuteuliwa au kuchaguliwa.
• Katiba Mpya iweke msingi wa kuweza kutambua michango ya wanawake katika kuendeleza rasilimali watu, kazi wanazofanya bila kutambuliwa nakupewa nyenzo na ulinzi wa afya zao
• Ulinzi kwa wanawake na watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia
• Katiba mpya iweke misingi ya kumwezesha mwananmke mwanamke kufikia , kufaidi huduma za msingi za jamii kama afya , elimu, maji safi na salama, chakula na makazi
• Katiba Mpya itambue haki za kila Mtanzania mwanamke kwa mwanamume kupata hifadhi ya jamii
Kutokana na umuhimu wa madai haya, tunadai mazingira wezeshi yenye itikadi inayozingatia ustawi wa wananchi walio wengi kutetea na kudai haki zao pamoja, uwepo wa uwajibikaji wa mihimili yote mitatu na uwajibikaji wa wananchi wote wanawake na wanaume na uwepo wa rasilimali za nchi zinazowanufaisha wananchi wote.
Sisi wanawake tumeweka mikakati madhubuti kuhakikisha sauti na madai yetu yanaingizwa katika Katiba mpya. Tukihamasishana:- kukubaliana kuhusu misingi mikuu ( kuwa na uelewa wa pamoja na sauti moja), ushiriki wa kutosha kwenye mikutano ya tume, Kushiriki kikamilifu kwenye mabaraza ya katiba ya kata na wilaya, kudai usawa katika uundaji wa bunge la katiba yanayoundwa, ushiriki katika kura za maoni, kutumia njia zilizowekwa za kufikisha ujumbe kwa tume, kuhamasisha wanawake washiriki kila hatua zote ya mchakato wa kuandaa katiba mpya.
Tunatumia nafasi hii kuwakaribisha wanawake , wanaume, wazee, vijana na jamii nzima kushiriki tukio hili muhimu na la kihistoria litakalofanyika katika viwanja vya TGNP siku ya Jumatano tarehe 08, 2013 saa 4:00 asubuhi
Tunawakaribisha sana na Ahsanteni kwa kutusikiliza!!!