TGNP Yafanikiwa Kuwatoa Wapangaji ‘Ving’ang’anizi’ Kwenye Jengo Lao

Baadhi ya wapangaji ving’ang’anizi wakiondolewa kwa nguvu kutoka katika jengo la TGNP ambalo lilikuwa na kesi

Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Usu Mallya akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari kutoa ufafanuzi juu ya TGNP kushinda kesi hiyo.

Wapangaji hao wakipakia mizigo yao kwenye gari tayari kwa kuiondoa eneo la jengo baada ya kuondolewa kwa nguvu.

Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com Dar es Salaam

MTANDAO wa Jinsia Nchini Tanzania (TGNP) leo umefanikiwa kuwaondoa kwa nguvu wapangaji ving’ang’anizi ambao walishindwa kesi ya kuligombea jengo la ghorofa moja lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam.

Jengo hilo ambalo TGNP ililinunua toka kwa mfilisi wa iliyokuwa Tanzania Sewing Thread Manufacturers Limited (TSTML) yaani Benki ya Rasilimali ya Tanzania (TIB) mwaka 1997 lilikuwa likigombewa na wapangaji 21 ambao walifungua kesi Mahakama Kuu kupinga mchakato wa uuzwaji wa jengo hilo kwa TGNP.

Zoezi la kuwaondoa wapangaji hao limefanywa na dalali wa Mahakama, Mamba (Mamba Auction Mart) kwa niaba ya TGNP chini ya ulinzi mkali wa polisi, ambapo wapangaji waliogoma kuondoka wenyewe baada ya kushindwa kesi walitolewa vyombo vyao nje ya jengo hilo na kuamriwa waondoke.

Mmoja wa maofisa wasaidizi kutoka kampuni ya udalali ya Mamba (katikati anayezungumza kwenye vinasa sauti) akitoa ufafanuzi kwa wanahabari kutoka vyombo anuai kuhusiana na kazi yao ya kuwaondoa kwa nguvu wapangaji hao.


Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wafanyakazi wa kampuni ya udalali ya Mamba wakitoa vyombo vya wapangaji nje ya jengo huku gari za polisi mbili zikiwa na baadhi ya askari wenye silaha na mabomu ya machozi zikiwa nje ya jengo hilo kuhakikisha hakuna anayegomea amri ya mahakama.

Kuondolewa kwa nguvu kwa wapangaji hao kumekuja mara baada ya Jaji wa Mahakama Kuu, Jaji Mwaikugile Machi 13, 2013 kutupilia mbali maombi ya wapangaji hao na kuwataka waondoke mara moja.

“…Leo hii zoezi linalotekelewa ni kutimiza amri ya Mahakama Kuu ya Machi 13, 2013 na amri ya mahakama ya kumpa ruhusa dalali wa mahakama Mamba Auction Mart, na zoezi linafanyika chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi kama mahakama ilivyoamuru,” inaeleza taarifa ya TGNP.

Akizungumzia tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Bi. Usu Mallya alisema wanashukuru kuona haki imetendeka na taasisi yao kuachiwa jengo hilo ambalo walilinunua kihalali kutoka kwa mmiliki. Alisema TGNP italitumia jengo hilo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kutanua wigo wa taasisi zake za mafunzo ya kijinsia kwa jamii ikilenga kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zao kudai na kulinda rasilimali ili kujiletea maendeleo.

Aliongeza kuwa wapangaji hao wamekuwa wakilitumia jengo hilo takribani kwa miaka 16 bila kulipia gharama za huduma kama za maji na nyinginezo, huku baadhi ya wapangaji kuwapangisha wapangaji wengine kinyemela na kujipatia fedha.