TGNP Mtandao tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha mwanahabari na mhariri Edson Kamukara kilichotokea jioni ya Tarehe 25.06.2015 jijini Dar es salaam. Kutoweka kwake ni huzuni kubwa kwetu, wanahabari na jamii kwa ujumla. Hakika taifa limempoteza mtu makini na mzalendo.
Kwa muda mrefu, TGNP Mtandao imefanya kazi na marehemu Kamukara katika kuihabarisha jamii na wanawake wa pembezoni wanapata taarifa na kupata nafasi ya kupaaza sauti zao. Ni dhahiri kuwaKamukara alikuwa mmoja wa wahariri tulio wategemea katika harakati za kumkomboa mwanamke. Alionesha moyo wa pekee wa kupenda kujitolea kuhakikisha anasaidia kusukuma mbele harakati za kutetea haki za wanyonge hasa migogoro ya ardhi vijijini, ukatili wa kijinsia na kutetea ajenda yetu ya kuwezesha wanawake kushika nafasi za uongozi katika ngazi zote.
Marehemu Kamukara alikuwa mwanaharakati, mtetezi wa wanyonge ambaye alijitahidi kuhakikisha sauti za makundi yaliyoko pemeboni zinasikika hata kwa gharama zake binafsi ili mradi ahakikishe wanawake na wanaume masikini wanapata fursa ya kumiliki rasilimali zao na kuifurahia keki ya taifa kwa usawa.
Tumemfahamau Edsoni kama mtu aliyechukia kabisa ubaguzi, unyonyaji, uonevu na uporaji wa rasilimali za wanyonge. Tumeshirikiana nae karibu sana katika kutetea wanawake wa vijini wapate maji salama na huduma nzuri za afya, makala zake zimejieleza wazi kazi nzuri aliyoifanya. Tutamkumbaka daima kwa kazi nzuri aliyoiacha.
Sisi tuliobaki hatuna budi kusheherekea mafanikio makubwa ambayo Kamukara aliyafanya kwa kupigania haki za wananchi na kuetetea demokraisa na haki za binadamu nchini. Tunawaomba wanahabari waendeleze kazi nzuri aliyoifanya Edson Kamukara wakati wa uhai wake. Tunatoa salamu zetu za rambirambi kwa familia yake, Mke, mtoto mama mzazi, wahariri wote na wanahabari na ndugu wengine pole sana kwa msiba huu mzito. Tunawaombea faraja katika kipindi hiki kigumu.
Imetolewa na
……………..
Lilian Liundi
Mkurugenzi wa TGNP Mtandao