TFF Yachunguza Kifo cha Mchezaji wa Mbao fc

333

KAMATI ya Tiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), inafanyia uchunguzi kifo cha mchezaji wa Mbao FC, Ismail Mrisho Khalfan aliyefariki jana wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 mjini Bukoba.

Taarifa ya TFF imesema kwamba Kamati hiyo inaendelea na uchunguzi wa kifo cha mchezaji huyo kabla ya baadaye kutoa taarifa za kamili ya kitatibu kujua juu ya kifo cha mchezaji huyo ambaye mwili wake umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mkoa Kagera.

Ismail Mrisho Khalfan alifariki dunia jana jioni mjini Bukoba baada ya kuanguka uwanjani dakika ya 74 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba dakika chache baada ya kuifungia bao timu yae katika ushindi wa 2-0

Alianguka baada ya kugongana na mchezaji wa Mwadui na baada ya kupatiwa huduma ya kwanza na kuonekana hali yake si ya kawaida, alikimbizwa hospitali ya mkoa wa Kagera kwa matibabu zaidi, ambako umauti ulimfika.

Mchezaji huyo amefariki akiwa ana umri wa miaka 19 na akiwa ametoka tu kufanya mtihani wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari ya Mwanza, maarufu ‘Mwanza Seco’.

TFF imesema imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha kushitukiza cha mchezaji huyo na inawapa pole wazazi wake, familia yake kwa ujumla, wachezaji wenzake, wanafunzi wenzake wa Mwanza Seco na kwa ujumla familia ya soka.

Mbao ipo kituo cha Bukoba mkoani Kagera kushiriki Ligi ya vijana ambayo kwa msimu huu imefanyika kwa mara ya kwanza, kundi lingine likiwa Dar es Salaam. Mungu ampumzishe kwa amani kijana Ismail Mrisho Khalfan
Chanzo:binzubeiry.co.tz