SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezindua rasmi Mpango wa Maendeleo wa Mpira wa Miguu (Technical Development Plan- TDP) wa 2013-2016 ambao pamoja na mambo mengine unahusisha kutazama upya mfumo wa mashindano na kuunda kanda kwa ajili ya kusimamia maendeleo.
Uzinduzi huo umefanywa leo (Aprili 4 mwaka huu) na Rais wa TFF, Leodegar Tenga katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washirika mbalimbali wakiwemo wachezaji, viongozi wa mpira wa miguu, Serikali, klabu na Wahariri wa Michezo.
Rais Tenga amesema mpango huo unafuatia ule wa 2004-2007, na 2008-2012 ambayo ilitengenezwa kwa msaada wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). Mpango wa sasa umetengenezwa na TFF kwa kufuata mpango mfano (standard plan) wa FIFA.
Amesema mpango wa sasa ni wa kiufundi zaidi kwa vile umelenga kuendeleza mpira wa miguu, kwani iliyotangulia ilihusisha zaidi kutengeneza muundo wa TFF, kazi ambayo imekamilika kwani sasa shirikisho lina vyombo mbalimbali vya kusimamia mchezo huo.
“Wakati ule tulikuwa na Ligi Kuu tu, lakini tumeongeza mashindano ya aina mbalimbali kama U17, U20, Kombe la Taifa na sasa michuano ya Copa Coca-Cola itakuwa ya U15. Pia tukatengeneza Kanuni za Fedha, kilichomo katika mpango wa sasa ni kujenga mpira. Chombo (TFF) tayari kipo,” amesema.
Rais Tenga amesema TFF imefika hapa kutokana na watu kujitolea ambapo ametaka moyo huo uendelezwe, lakini akasisitiza washirika wote kuwa na mpango huo na kuusoma kwani umetokana na maoni yao ambapo kila mmoja ana kazi ya kufanya katika mpango huo.
“Naomba washirika wote wasome mpango huu. Kama mtu una mawazo zaidi baada ya kusoma, toa maoni yako. Mpango huu si Msahafu, utabadilika kutokana na maoni ya watu. Kama una mawazo zaidi, toa maoni yako kwa lengo la kujenga, isiwe kazi ya kulaumu tu kuwa mpango una upungufu. Mabadiliko yanafanyika kutokana na mawazo mapya,” amesema.
Amesema maendeleo ya mpira wa miguu ni mchakato mrefu, kwa hiyo unahitaji ushiriki wa watu kutokana na ukweli kuwa uongozi wa mpira wa miguu Tanzania bado ni wa kujitolea. Rais Tenga amesema ahadi ya TFF ni kushirikiana na washirika mbalimbali kuhakikisha kuna maendeleo kwa faida ya mpira wa miguu wenyewe na nchi kwa ujumla.
Amewashukuru wote waliotoa maoni kwa ajili ya mpango huo wenye kurasa 76. Mpango huo ulioandaliwa na Mkufunzi wa FIFA, Henry Tandau, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Ofisa Maendeleo wa TFF, Salum Madadi unapatikana kwenye CD na nakala laini (soft copy).