TFF yaweka hadharani uhamisho wa wachezaji mbalimbali

UHAMISHO WA WACHEZAJI 2011/2012

Uhamisho wa wachezaji wa Ligi Kuu kwa msimu wa 2011/2012 ulifikia tamati jana
saa 6 kamili usiku. Wachezaji ambao maombi yao ya uhamisho yamewasilishwa TFF ni
Shabani Kado kutoka Mtibwa Sugar kwenda Yanga, Salum Machaku kutoka Mtibwa Sugar
kwenda Simba na Idrisa Rajab kutoka African Lyon kwenda Yanga.

Hao ni kwa wachezaji ambao maombi yao yametumwa kwa njia ya barua. Kwa vile
uhamisho vile vile unaweza kufanywa kwa njia ya mtandao (Transfer Match System-
TMS), uhamisho mwingine uliofanyika utafahamika kesho baada ya Kurugenzi ya
Mashindano kupitia mfumo huo wa TMS ambao klabu zote za Ligi Kuu tayari zina
namba zao maalumu za kuingia (passwords).

WACHEZAJI WALIOTOLEWA KWA MKOPO
Wachezaji waliotolewa kwa mkopo kutoka Simba kwenda klabu zingine ni Aziz Gilla
na Mbwana Bakari (Coastal Union), Mohamed Kijuso, Mohamed Banka na Haruna Shamte
(Villa Squad), Meshack Abel (Ruvu Shooting), Juma Jabu, Andrew Kazembe, Paulo
Terry na Godfrey Wambura (Moro United).

Kutoka Azam ni Sino Augustino na Selemani Kassim ambao wanakwenda African Lyon,
na Tumba Louis (Moro United). Yanga imewapeleka wachezaji wake Omega Seme na Idd
Mbaga kwa mkopo African Lyon.

MORO UNITED KUCHEZA CHAMAZI
Klabu ya Moro United imewasilisha barua ya kutumia Uwanja wa Azam ulioko
Chamazi, Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom. Nayo Villa
Squad imeomba kutumia uwanja huo huo, ingawa bado haijaonesha barua kutoka Azam
inayowaruhusu kutumia uwanja wao.

Klabu ya African Lyon ndiyo pekee ambayo bado haijawasilisha uwanja ambao
itautumia kwa ajili ya ligi hiyo itakayoanza Agosti 20 mwaka huu. Kwa Lyon
kushindwa kuleta jina la uwanja wake hadi sasa inasababisha TFF kuchelewa kutoa
ratiba ya ligi, hivyo tunaitaka Lyon kutimiza wajibu wake katika suala hilo
haraka.

Boniface Wambura
Ofisa Habari