TFF yatupilia mbali pingamizi la Yanga dhidi ya Simba

KAMATI haikusikiliza pingamizi la Yanga dhidi ya Simba kuhusu wachezaji iliyotoa kwa mkopo baada ya kubaini kuwa wachezaji ambao Simba imewatoa kwa mkopo ni wane tu; Haruna Shamte (Villa Squad), Aziz Gilla (Coastal Union), Ahmed Shiboli (Kagera Sugar) na Mohamed Kijuso (Villa Squad).

Wachezaji wengine waliotajwa na Simba kupelekwa kwa mkopo katika klabu mbalimbali ilibainika kuwa ni wa kikosi cha pili (U20) ambao hawahusiki na kanuni ya mkopo. Wachezaji wanaoweza kutolewa kwa mkopo ni wa kulipwa tu (wenye mikataba).

Kwa upande wa Athuman Idd na Juma Jabu ambao hawakuonekana kwenye orodha ya usajili ya Simba, kamati imesema ni wachezaji halali wa klabu hiyo kwa vile wana mikataba nayo. Idd ana mkataba wa miaka miwili wakati Jabu mkataba wake umebakiza mwaka mmoja kumalizika. Kamati imesisitiza kuwa kitu kikubwa kinachoangaliwa kwenye usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ni mikataba na si kusaini fomu za usajili.

Kuhusu Amani Kyata, aliombewa usajili katika klabu mbili za African Lyon na Yanga. Lyon walimuombea kwa timu ya wakubwa, wakati Yanga walimuorodhesha katika timu ya pili (U20).

Kamati ilibaini kuwa mchezaji huyo ni wa kituo cha Tanzania Soccer Academy (TSA) kinachomilikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na hakuna mchakato wowote uliofanyika kumsajili, hivyo usajili wake haujakamilika Yanga wala Lyon.

SUALA LA MCHEZAJI OSCAR JOSHUA
Sekretarieti ya TFF imeelekezwa kupeleka suala la mchezaji huyo Polisi kwa ajili ya uchunguzi kwa vile kuna barua mbili zinazopingana kutoka timu yake ya Ruvu Shooting- ya kwanza ikiridhia achezee Yanga na ya pili ikipinga kuwa taratibu hazikufuatwa katika kujiunga na timu yake mpya.

Uamuzi huo wa kamati umelenga kubaini ipi ni barua halali kati ya mbili zilizowasilishwa TFF kuhusu usajili wake Yanga, na zote zikionesha kutoka katika timu yake ya Ruvu Shooting.

Pia kamati imeamua kuwa kwa vile TFF ilifanyia kazi barua ya kwanza ya kumruhusu kwenda Yanga, hivyo kumpatia leseni, mchezaji ataendelea kutumia leseni hiyo hadi taarifa ya uchunguzi wa Polisi kuhusiana na barua hizo mbili itakapotolewa.

HARUNA MOSHI v POULSEN
Kuhusu mchezaji Haruna Moshi ‘Boban’ kutoitikia mwito wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen kucheza mechi kati ya U23 na Shelisheli zilizofanyika Arusha, kamati kwa sasa imeliacha suala hilo kwa kocha huyo kwa vile kuna maagizo ametoa kwa mchezaji huyo.

Poulsen amemtaka Boban binfasi kwenda kumueleza sababu ya kutoitikia mwito wake wa kucheza mechi dhidi ya Shelisheli kabla hajafanya uamuzi mwingine kuhusu mchezaji huyo.

Imetolewa na Boniface Wambura, Ofisa Habari, TFF.