TFF Yatuma Rambirambi Vifo vya Rais Sata na Meyiwa

kipa wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Senzo Meyiwa.

kipa wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Senzo Meyiwa.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewatumia salamu za rambirambi vyama vya mpira wa miguu vya Zambia (FAZ) na Afrika Kusini (SAFA) kutokana na vifo vya Rais Michael Sata na kipa wa timu ya Taifa ya Afrika Kusini, Senzo Meyiwa.
 
Ametuma salamu hizo kwa Rais wa FAZ, Kalusha Bwalya na Rais wa SAFA, Danny Jordan na kuongeza kuwa amepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya ghafla vya Rais Sata na kipa huyo wa Bafana Bafana vilivyotokea wiki hii. Rais Malinzi amesema kuwa misiba hiyo si pigo kwa Zambia na Afrika Kusini pekee bali Afrika kwa ujumla kwa vile walikuwa na mchango mkubwa kwa ustawi wa mchezo wa mpira wa miguu.
 
Amewaomba Rais Jordan na Rais Bwalya kutuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya Sata, na familia ya Meyiwa, na kuzitaka kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha misiba hiyo mizito kwao. Rais Sata (77) alifariki dunia juzi kwenye Hospitali ya King Edward VII nchini Uingereza alipkuwa kwenye matibabu, wakati kipa Meyiwa aliuawa kwa kupigwa risasi Jumapili mjini Vosloorus.

SDL KUANZA KUTIMUA VUMBI NOVEMBA 22
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 zitakazocheza katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu.
 
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyoketi jijini Dar es Salaam jana (Oktoba 29 mwaka huu) chini ya Mwenyekiti wake Geofrey Nyange ilipitia maandalizi maandalizi ya ligi hiyo ikiwemo mwongozo wake (roadmap).
 
Kwa mujibu wa mwongozo huo, usajili wa wachezaji utamalizika Oktoba 31 mwaka huu. Kipindi cha pingamizi ni kuanzia Novemba 1 hadi 7 mwaka huu wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajia kukutana Novemba 11 mwaka huu kwa ajili ya kupitisha usajili. Pia Kamati ya Mashindano imepitisha viwanja vya timu zote, isipokuwa uwanja wa timu ya Mpanda United ya Katavi na ule wa Town Small Boys ya Tunduru mkoani Ruvuma.
 
Uwanja wa Town Small Boys haukupitishwa kwa vile hauna uzio wa kudumu ( wa chuma) wa kutenganisha wachezaji na washabiki, na pia ufikaji wa timu Tunduru ni mgumu kutokana na ubovu wa barabara ikizingatiwa kuwa ligi hiyo itachezwa hadi kipindi cha Masika.
 
Kwa upande wa uwanja wa Mpanda United, umekataliwa kwa vile hauna vigezo vya msingi vinavyotakiwa ikiwemo vyumba vya kubadilishia nguo, kutokuwa na nyasi na uzio wa kudumu kutenganisha wachezaji na washabiki. Kutokana na uamuzi huo, Mpanda United sasa itatumia Uwanja wa Mandela uliopo Sumbawanga wakati Town Small Boys itachezea mechi zake kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.