TFF Yatoa Pole Msiba wa Gebo Peter, Kanali Ali Mwanakatwe

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura


SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa zamani wa timu ya Simba na Taifa Stars, Gebo Peter kilichotokea usiku wa Juni 6 mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
 
Gebo aliyezaliwa mwaka 1961, pia aliwahi kuchezea timu za Sigara ya Dar es Salaam, CDA ya Dodoma na kombaini ya Mkoa wa Dar es Salaam (Mzizima United). Hadi mauti yanamkuta alikuwa akijishughulisha na biashara, kubwa ikiwa ya vifaa vya michezo.
 
Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu nchini kwani, Gebo enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa mchezaji na baadaye kiongozi katika timu ya Manyema ya jijini Dar es Salaam.
 
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Gebo Peter, klabu ya Manyema na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
 
Msiba upo nyumbani kwao Vingunguti karibu na Kanisa Katoliki ambapo taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia.
 
Marehemu ambaye ameacha mjane na watoto watatu anatarajiwa kuzikwa kesho (Juni 7 mwaka huu) nyumbani kwao Kigurunyembe, mjini Morogoro. Bwana alitoa, na Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Amina

RAMBIRAMBI MSIBA WA KANALI MWANAKATWE

Wakati huo huo, TFF imepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe kilichotokea leo asubuhi (Juni 7 mwaka huu) katika Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba yake alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika wakati madaktari wakimpatia matibabu.
 
Kanali Mwanakatwe alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani. Baada ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kufanikiwa kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.
 
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani, Kanali Mwanakatwen enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi kuwa Kamishna wa CAF.
 
TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na hoteli ya Giraffe wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani. TFF tunasubiri taratibu hizo ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo. Sisi sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea.