TFF yataja viingilio Nigeria Vs Tanzania U 23

Mechi ya kwanza ya mchujo ya michuano ya Olimpiki kati ya timu ya Taifa ya
Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23 dhidi ya Nigeria itafanyika
Jumapili (Juni 5, 2011) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 kamili
jioni.
 
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 1,000 kwa viti vya kijani, bluu na rangi ya chungwa (orange straight and curve), sh. 5,000 kwa VIP ‘C’ na ‘B’ na sh.
10,000 kwa VIP ‘A’. Tiketi zitaanza kuuzwa Ijumaa saa 2 asubuhi kwenye vituo vya Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa, Bigbon Msimbazi (Kariakoo), Steers (Mtaa wa Ohio na Samora), Uwanja wa Uhuru, Ubungo OilCom na vituo vya mauzo vya Premier Sports Betting.

Nigeria itawasili Juni 3 mwaka huu kama ilivyo kwa waamuzi wa mechi hiyo kutoka Kenya na Kamishna kutoka Ethiopia. Mwamuzi ni Sylvester Kirwa ambaye atasaidiwa na Peter Kiereini, Aden Marwa na Davies Omweno wakati Kamishna ni Sahilu Gebremariam.
 
Pia TFF kupitia Kurugenzi ya Masoko imepiga marufuku wachuuzi wa viburudisho kwenye mechi hiyo, isipokuwa kwa kampuni maalumu iliyopewa kazi hiyo. Hivyo vijana wote watakaofanya biashara bila kibali cha TFF watakamatwa. Suala hili pia linawahusu wachuuzi wa jezi za timu ya Taifa uwanjani.
 

Wakati huo huo TFF pia imetoa kalenda yake ya matukio kwa mwaka 2011/2012 ambapo kipindi cha kwanza cha matayarisho ya msimu kinaanza Juni 1 hadi Agosti 13 mwaka huu. Kipindi cha kwanza cha uhamisho kinaanza Juni 1 hadi Julai 15 ambapo usajili wa kwanza utakuwa Juni 1 hadi Julai 20.
 
Kutangaza wachezaji wa kuachwa/kusitisha mikataba ni kuanzia Juni 1 hadi 21
mwaka huu wakati kupitia majina na kutangaza pingamizi ni kati ya Julai 21-31
mwaka huu.
 
Kipindi cha pili cha uhamisho kitaanza Novemba 1 hadi 20 mwaka huu wakati
usajili utaanza Novemba 1 hadi 30 mwaka huu. Ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom
inatarajiwa kutoka Julai 20 mwaka huu. Ngao ya Hisani kwa ajili ya ufunguzi wa
msimu kwa mikoa yote itachezwa Agosti 13 mwaka huu wakati mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom utaanza Agosti 20 mwaka huu.
 
TFF tunawaomba wadau wote kuhakikisha wanapata kalenda hii ili waweze kupanga shughuli na mipango yao kwa kuizingatia.