TFF yataja viingilio mechi ya Twiga Stars na Namibia

Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Wanawake 'Twiga Stars' ya Tanzania

KIINGILIO cha chini kwa mechi ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) kati ya Twiga Stars na Namibia itakayochezwa Jumapili, Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 2,000.

Kiwango hicho ni kwa washabiki kwa viti vya bluu na kijani. Viti hivyo kwa pamoja vinachukua jumla ya watazamaji 36,693 kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua washabiki 60,000.

Pia kutakuwa na kiingilio cha watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 ambacho ni sh. 1,000. Watoto watakaotumia tiketi hizo wanatakiwa kuingia uwanjani wakiwa na wazazi au walezi wao.

Viingilio vingine kwa mechi hiyo ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 5,000 kwa VIP B na C n ash. 10,000 kwa VIP A. Namibia inatarajia kuwasili nchini Januari 27 mwaka huu saa 12.45 jioni kwa ndege ya South Africa Airways.

Wakati huo huo, Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho madogo kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom kutokana na Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kutumika kwa sherehe za kitaifa za kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mechi namba 111 kati ya Toto Africans na African Lyon ambayo kwa mujibu wa ratiba ilikuwa ichezwe Februari 5 mwaka huu Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza sasa itachezwa Aprili 18 mwaka huu.

Mabadiliko hayo yamefanyika baada ya wamiliki wa Uwanja wa CCM Kirumba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kueleza kuwa watautumia kwa sherehe za kuzaliwa chama chao, hivyo hautakuwa na nafasi kwa Februari 4, 5 na 6 mwaka huu.

Uamuzi huo umesababisha pia mabadiliko kwa mechi nyingine mbili. Mechi namba 168 kati ya Villa Squad na African Lyon iliyokuwa ichezwe Aprili 18 mwaka huu Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam, sasa itachezwa Aprili 22 mwaka huu.

Pia mechi namba 170 kati ya Azam na Toto Africans iliyokuwa ichezwe Aprili 29 mwaka huu jijini Dar es Salaam sasa imerudishwa nyuma hadi Aprili 26 mwaka huu ambayo ni Sikukuu ya Muungano.