KAMATI ya Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF limetangaza Uchaguzi Mkuu wa klabu ya Coastal Union ya jijini Tanga utafanyika tarehe 05, Julai 2015. Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Melchesedek Lutema ametoa ratiba ya mchakato mzima wa uchaguzi huo, ambapo tarehe 21-22 Mei mwaka huu zitatangazwa nafasi zote zinazogombewa.
Kwa mujibu wa kalenda hiyo ya Uchaguzi, tarehe 23-30, Mei 2015 itakua ni kipindi cha uchukuaji fomu kwa wagombea wote na kuzirudisha, wakati Juni Mosi mpaka Juni 04, 2015 ni kipindi cha mchujo wa awali kwa wagombea.
Juni 05, 2015 Kamati ya Uchaguzi itatoa orodha ya awali ya wagombea, Juni 7-9, 2015 itakua ni kipindi cha kupokea na kuweka pingamizi kwa wagombea, na Juni 10-11 ni kupitia mapingamizi yote.
Julai 02 -04, 2015 ni muda wa kampeni kwa wagombea wote na uchaguzi mkuu utafanyika tarehe 05, Julai 2015. Ratiba kamili ya mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Coastal Union imeambatanishwa.
Wakati huo huo, Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inashuka dimbani kucheza mchezo wake wa pili dhidi ya timu ya Taifa kutoka Madagascar, mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Royal Bafokeng majira ya saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Taifa Stars inahitaji kupata ushindi katika mchezo wa leo dhidi ya Madagascar ili kufufua matumaini ya kuweza kusonga mbele katika hatua inayofua ya Robo Fainali. Kocha Mkuu wa Taifa Stars akiongelea mchezo wa leo amesema, makosa yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Swaziland yamefanyiwa kazi na anaamini vijana wake watafanya vizuri.
“Mchezo wa Swaziland tulipata nafasi nzuri za kufunga, lakini washambuliaji wangu hawakuwa makini kuzitumia nafasi hizo, tatizo la kupoteza nafasi nyingi limefanyiwa kazi na nina amini leo vijana watafanya vizuri” alisema Nooij.
Aidha Nooij amesema anataarajia mchezo kuwa mgumu kutokana na Madagascar kuhitaji ushindi wa pili mfululizo, baada ya kuifunga Lesotho katika mchezo wa awali, Nooij ameahidi kufanya vizuri katika mchezo huo. Mchezo huo utakuwa moja kwa moja (Live) katika kituo cha Superspot SS4, na SS9.
Naye kiungo wa Taifa Stars, Said Juma Makapu anarejea nyumbani leo usiku kwa usafiri wa Shirika la ndege la Fastjet kwa ajili ya kufanyia vipimo zaidi na matibabu, anatarajiwa kuondoka uwanja wa O.R. Tambo saa 5 usiku kufika uwanja wa JK Nyerer saa 8 usiku.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)